Viongozi vyama vya siasa wawapa neno Mbowe, Lissu

VIONGOZI wa vyama vya viasa na wachambuzi wa siasa wamewashauri viongozi wapya wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA) kuhakikisha wanarejesha umoja na mshi[1]kamano kati ya wananchama ili kukiimarisha. Kadhalika, wamewapongeza kwa kuendesha uchaguzi wao kwa uhuru na uwazi na kuwataka kurekebisha udhaifu uliopo kwa kurekebisha katiba yao.
Akizungumza na HabariLEO jana, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Hatibu alisema mwenyekiti mpya wa Chadema, Tundu Lissu anapaswa kuwaongoza wanachama kushikamana ili kukijenga zaidi chama chao.
“Anachotakiwa kufanya, Lissu ni kuwaunganisha wanachama wote, waondoe makundi pia watengeneze katiba yao hasa katika eneo la muda wa viongozi, wakati mwingine haipendezi sana mwenyekiti kukaa muda mrefu sana,” alisema. Pia, alieleza kwamba uchaguzi wa Chadema ulikuwa wa uwazi na demokrasia ilichukua nafasi yake.
Alisema vyama vingine vina mengi ya kujifunza kutoka kwao kutokana na ushirikishwaji na uwazi ulioonekana. Alimpongeza mwenyekiti wa Chadema aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe kukubali matokeo na kwamba ni ukomavu wa kisiasa ambao viongozi wengine wa Afrika wanatakiwa kuchukua kama funzo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya alisema, Lissu atahitaji watu wenye uzoefu mkubwa wa uongozi ndani ya chama hicho kama, Mbowe kumshauri ili kufanya chama kizidi kuimarika.
“Mbowe kukosa uenyekiti hakumnyimi nafasi zake nyingine katika chama, atakuwa mshauri namba moja wa chama kwa sababu kama asipotoa ushirikiano, Lissu mwenyewe itamuwia vigumu kuongoza chama,” alifafanua.
Kwa upande wake, Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha ACT-Wazalendo, Salim Bimani alisema Chadema wameonesha kuwa sasa ni muda wa kukuza demokrasia nchini. Aidha, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa ku[1]pitia mitandao yao ya kijamii walitoa pongezi kwa Lissu.
Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alisema kuchaguliwa kwa Lissu kunamfanya pia, awe Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), akiwa Makamu Mwenyekiti. Alimkaribisha katika uongozi wa TCD.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, aliandika: ‘Ushindi wako unadhihirisha imani kubwa waliyonayo wanachama wa chama chako kwako. Nakutakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yako na nina imani kubwa kuwa tutashirikiana katika harakati za kupigania demokrasia hapa nchini na kuwaletea Watanzania mabadiliko wanayoyataka’.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zanzibar Ismail Jussa alimpongeza kwa kuchaguliwa kuongoza wana Chadema na kwamba anamtambua, Lissu kama mtu jasiri na mwenye msimamo katika kusimamia kile anachokiamini.
Aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto alimpongeza, Mbowe kwa ushindani aliotoa katika mchakato wote wa uchaguzi na kwa mchango wake katika siasa na mageuzi ya Tanzania. “Nakukaribisha mweyekiti mstaafu, Mbowe katika ustaafu na kukuhakikishia kuwa kuna mengi ya kufanya nje ya siasa za uongozi katika kazi kubwa iliyo mbele yetu ya kujenga na kustawisha demokrasia ya nchi yetu ambayo inatuhitaji wana mageuzi wote walio ndani na nje ya uongozi,” alisema Zitto



