‘Chuma cha Chuma’ atupwa jela miaka mitatu

DAR-ES-SALAAM : MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu kama ‘Chuma cha Chuma’, ambaye ni raia wa Burundi, kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Shilingi 500,000 baada ya kukutwa na hatia ya kuishi nchini Tanzania bila kibali, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Februari 5, 2025, na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa.
Ndikuriyo, ambaye ni msanii maarufu wa muziki, alikamatwa kwa kosa hilo Septemba 18, 2024, katika eneo la Las Vegas Casino, Upanga wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.
Hakimu Ruboroga alisema kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya pili na kwamba anahitaji kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wanaojihusisha na vitendo kama hivyo.
SOMA: Kiongozi upinzani afunguliwa kesi mauaji



