Barrick yachangia tril 3.6/- Serikalini miaka 4

KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Barrick imechangia shilingi trilioni 3.6 katika mapato ya Serikali kupitia kodi, mrabaha na tozo mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024.
Meneja Mkaazi wa Kampuni hiyo hapa nchini Dk Melkiory Ngido amesema hayo jijini Dodoma mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akiwasilisha Maendeleo ya Kampuni Tanzu Baona ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania inayofamika kama Twiga Minerals.

Dk Ngido ameelezea kuwa, kwa mujibu wa takwimu za miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, Kampuni Barrick imewekeza zaidi ya dola bilioni 4.24 (Tsh trilioni 11) katika shughuli zake ndani ya nchi, huku dola bilioni 1.5 (Tsh trilioni 3.6) zikilipwa serikalini kupitia kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali.

Amesema Kampuni ya Barrick ilipochukua usimamizi wa shughuli zake Tanzania mwaka 2019, kampuni hiyo imeendelea kuwa mdau mkubwa wa uchumi kupitia uwekezaji, ajira, na miradi ya kijamii.
Dk Ngido ameelezea kuwa Dola za Marekani milioni 158 (shilingi bilioni 412.4) sawa na asilimia 4 zimelipwa kama gawio la Serikali kutoka na ubia huo.

Sambamba na hilo, Dk Ngido amesema Dola bilioni 2.3 (shilingi trilioni 6.04) sawa na asilimia 55 ya matumizi yote yameelekezwa kwa wasambazaji wa ndani, huku asilimia 32 ya uwekezaji huo dola bilioni 1.37 (shilingi 3.57) kimelipwa kama kodi, mrabaha, na tozo mbalimbali kwa serikali.

Ameongeza dola milini 397 milioni (shilingi trilioni 1,03) sawa na asilimia 9 zimetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi huku dola milioni 30 (shilingi bilioni 78.3) zikitumika kwenye utafiti wa madini katika maeneo hayo na dola milioni 15.6 sawa na shilingi bilioni 40.7 zimeelekezwa kwenye miradi ya kijamii.



