Wadau, TradeMark Africa wajadili ufanisi wa bandari

WADAU mbalimbali wa biashara ambao ni watumiaji wa Bandari ya Dar es Slaam ikiwemo Taasisi ya Trademark Afrika (TMA) wamekutana kujadili na kuboresha mifumo mbalimbali inayochangia kuimarika kwa mazingira ya biashara kupitia Bandari za Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Februari 22, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TradeMark Afrika, Sanjai Rhugani amesema wamejadili namna biashara Afrika inaweza kupanuka kupitia bandari za Tanzania.
“Lengo kuangalia jinsi biashara Afrika inaweza kuwa na wigo mpana kupitia Tanzania,” amesema Rughani.

Mkurugenzi wa Kanda Afrika Mashariki na Kati wa TradeMark Afrika, Monica Hangi akizungumza amesema taasisi yao imebeba kipaumbele cha serikali kuwaleta wafanyabiashara pamoja na kutumia Bandari za Tanzania.
Amesema pamoja na hilo, wadau katika kikao hicho wamepata maelekezo ya namna bandari inavyofanya kazi huku Mamlaka ya Bandari (TPA) ikipata mawazo chanya namna ya kuboresha utendaji kazi wa bandari kwa manufaa yao, wafanyabiashara na Tanzania pia.

“Lakini pia kuangalia jinsi TPA itakavyokuwa na uharaka katika kuhudumia bandari kwa biashara ili kuongeza ufanisi kiutendaji,” amesema Monica.

Aidha, Monica amesema TRA imehawahakikishia usalama wa bidhaa zinapofika bandarini na kwamba biadhaa zote zitakuwa katika usalama wa kutosha kwa kuzingatia kuwa TRA imeboresha mifumo ya ulinzi bandarini.
Akijibu hoja za wadau hao, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Abed Gallus amesema Bandari ya Dar es Salaam imeboresha utendaji wake ambapo kwa sasa meli za makasha zinasubiri siku tatu badala ya 30 awali ilivyokuwa.
Gallus amesifu hatua hiyo kuwa imetokana na mchango wa Trade Mark Africa katika kufanya tafiti mbalimbali za kuboresha upitishaji wa mizogo katika corido za bandari.

“Trade Mark wanatusaidia kutupa taarifa za kutosha ambazo zinatusaidia kubadilisha utendaji wetu wa kazi lakini kuboresha sehemu zenye mapungufu,” amesema Gallus.
Amesema zaidi ya kontena 1,000 zilizokaa muda mrefu zimepelekwa Bandari Kavu ya Kwala ili kupunguza shehena katika Bandari ya Dar es Salaam lengo likiwa kuhudumia shehena zingine.
“Wiki hii tutapeleka makontena 500 katika Bandari ya Kwala, mwitikio mzuri, wateja wanafurahia tunawawekea siku 60 bila kuwatoza,” ameongeza.

Edward Kalanje kutoka Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amesema wamefanya maboresho ya Mfumo Jumuishi wa Forodha Tanzania (TANCIS) lakini pia kutoa mafunzo namna ya kutumia mfumo huo.
“Tumewaonesha pia maboresho ambayo tumefanya ya mifumo ambao tumeanza kuutumia Januari 20, 2025, tumewaleza namna yatakavyokuwa na manufaa kwa maana yakupunguza muda wa kufanya ukaguzi ‘Clearence’ lakini kutumia mfumo wa dirisha moja ,” amesema Kalanje.

Santina Benson, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Taasisi ya Ethical Leadership For Growth and Prosperity amesema majadiliano yamekuwa na tija kwa wafanyabiashara kupata uelewa kati ya TPA na TRA ya masuala mbalimbali, lakini kuangalia namna ya kutatua changamoto.
“Lakini wafanyabiashara wapate kujiamini katika shughuli zao,” amesema Santina.



