Serikali yasisitiza uwazi, uadilifu vyama vya ushirika

DODOMA: SERIKALI imewataka viongozi wa vyama vya ushirika nchini kuendesha taasisi hizo kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu, huku ikionya kuwa haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaobainika kujihusisha na ubadhirifu wa fedha za wanachama.

Aidha, serikali imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri pamoja na waajiri wote wanaodaiwa fedha za makato ya wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuhakikisha wanazilipa kwa wakati, ikieleza kuwa kuchelewesha fedha hizo ni aina ya unyonyaji unaodhoofisha maendeleo ya sekta ya ushirika.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde wakati wa kufungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani 2026 kwa niaba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.

Alisema baadhi ya viongozi wanaotumia nafasi zao kujinufaisha kwa fedha za wanachama, akisema serikali haitavumilia vitendo vya ubadhirifu.

“Wapo wanaoingia kwenye vyama vya ushirika wakiona ni fursa ya kutumia fedha za wanachama kwa ubadhilifu. Serikali haitavumilia hilo, Sirikali itawanyoosha wote watakaohusika. Tutakamata viongozi wote wanaohusika na ubadhirifu na tutawafunga. Hatuna mchezo kwenye hili.”

Alisema serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa mara kwa mara katika vyama vya ushirika ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha wakulima wanapata manufaa ya ushirika.

Silinde alisema lengo la serikali ni kujenga ushirika imara unaowanufaisha wanachama, kuongeza thamani ya mazao, kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri kupitia mifumo ya kidijitali, kupunguza utegemezi, kukuza ajira na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la kimataifa.

Alisema serikali itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na wadau mbalimbali kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Silinde pia alisisitiza kuwa uwazi na uwajibikaji ndiyo msingi wa kujenga imani ya wanachama na wadau, akieleza kuwa vyama vinavyozingatia misingi hiyo vinakuwa mfano bora wa demokrasia ya kiuchumi na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Tito Haule, alisema sekta ya ushirika inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowakwamisha wanachama wake, ikiwamo mifumo ya kodi na upatikanaji wa mitaji.

Aliiomba serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002 ili iendane na mahitaji ya sasa ya sekta hiyo, pamoja na kuongeza mtaji wa mfuko huo ili kusaidia kutatua changamoto za masoko na ubora wa mazao.

Pia alipendekeza kiwango cha kodi ya mapato kwa vyama vya ushirika kipunguzwe kutoka asilimia 30 hadi asilimia 10 ili kuvipa uwezo mkubwa wa kuhudumia wanachama.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button