Nchi zinazozalisha kahawa zakubaliana mambo manne

NCHI 25 zinazozalisha kahawa Afrika zimekubaliana kushirikiana kufanya tafiti na kuongeza thamani ya zao hilo ili kupata mavuno bora na kukuza uchumi.
Aidha, nchi hizo zimeomba Umoja wa Afrika (AU) kushirikisha Shirika la Kahawa Afrika (IACO) unapokuwa unajadiliana masuala ya kahawa na Umoja wa Ulaya (EU).
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hayo aliposoma Azimio la Dar es Salaam katika mkutano wa tatu wa nchi zin[1]azozalisha kahawa Afrika G-25 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jana.
Azimio hilo lenye makubaliano manne lilipitishwa na viongozi wote wanachama waliohudhuria mkutano huo. Makubaliano mengine ni kusaidiana kwenye uwekezaji katika kuongeza thamani zao la kahawa na kuongeza matumizi ya ndani ya bidhaa hiyo.
“Pia, tumeazimia kuchakata na kufanya biashara ya kahawa angalau asilimia 50 ndani ya Afrika ifikapo 2035 na kubuni mbinu mpya za kiteknolojia katika mnyororo wa thamani wa kahawa,” alisema Bashe. Pia, wametaka kuanzishwa viwanda vya kuchakata kahawa katika nchi hizo na kuwe na kituo cha utafiti wa zao hilo Afrika.
“Serikali za Afrika ziunge mkono juhudi za kuongeza matumizi ya kahawa ya ndani lakini pia ziwezeshe raia wao kuwekeza katika sekta binafsi ili kulipa thamani zao la kahawa,” alisema Bashe.
Aidha, Azimio hilo lililosainiwa na Bashe na Mwenyekiti wa IACO na Waziri wa Kilimo na Mifugo wa Burundi, Prosper Dodiko limeazimia kufanyika kwa mkutano wa G-25 kila baada ya miaka miwili na kukubaliana mkutano ujao ufanyike Ethiopia mwaka 2027.
Wakizungumza kuhusu azimio hilo viongozi waliowakilisha nchi zao walisema kwa hali ili[1]yopo kwa sasa azimio halipingiki kwa kuwa limefanyika kwa manufaa ya Waafrika.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Kahawa la Afrika (IACO), ukiwa na kaulimbiu ya ‘Fungua fursa za ajira kwa vijana kupitia uimarishaji wa tasnia ya kahawa Afrika.’ Nchi 25 zinazozalisha kahawa Afrika ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, Cameroon, Zimbabwe, Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Zimbabwe. Nyingine ni Ivory Coast, Angola, Ghana, Guinea, Sierra Leone, Togo, Afrika Kusini, Algeria, Benin, Gabon, Equatorial Guinea, Liberia na Nigeria.



