Muhas waandaa kambi uchunguzi wa afya

CHUO Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeanda kambi maalum ya huduma za uchunguzi wa afya kuanzia Februari 26 hadi 27, 2025 itakayofanyika Kampasi ya Mloganzila saa 3:00 mpaka 10:00 jioni ili kuwapa wananchi nafasi ya kufanyiwa uchunguzi wa afya zao.
Akizungumza na waandishi wa habari hii leo, Makamu`Mkuu wa chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema uchunguzi huo utafanyika kwa magonjwa ya macho, masikio, pua na koo, kinywa meno, saratani ya matiti na shingo ya kizazi, homa ya Ini na tezi dume kwa kipimo cha damu.
Amesema sambamba na uchunguzi huo, wataalamu wa MUHAS watatoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa na usugu wa dawa mwilini, magonjwa ya kuambukiza, utengenezaji na ukarabati wa vifaa tiba, uchakataji wa taarifa za afya kwa kutumia akili mnemba na lishe.
Aidha, Prof Kamuhabwa amesema kutakuwa na maonyesho ya afya na elimu yatakayoonyesha mafanikio katika sekta ya afya na elimu, zikiwemo tafiti mpya, ubunifu wa kiteknolojia na juhudi zinazofanywa na chuo hicho kuboresha huduma za afya nchini.
“Washiriki watapata fursa ya kujifunza na kushuhudia jinsi teknolojia mpya inavyoboresha utoaji wa huduma za afya na elimu. Pia, kutatolewa huduma za siku zijazo na pia watapata huduma za bure kupima afya zao,” amesema Prof Kamuhabwa.
Katika kuimarisha zaidi mazingira ya mafunzo, huduma za afya na kuinua tafiti, chuo hicho kitaweka jiwe la msingi ujenzi wa Ndaki ya Tiba ‘College of Medicine’ na Shule ya Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika Kampasi ya Mloganzila.
“Mradi huu ni hatua kubwa kuelekea kupanua miundombinu ya chuo na hivyo kuongeza udahili wa wanafunzi na kuboresha ubora wa mafunzo kwa wanataaluma,” ameongeza Prof Kamuhabwa.



