Changamoto zinazouia mabadiliko halisi ya sera za kodi

KATIKA toleo lililopita, makala haya yalijikita katika uhusiano baina ya sera ya kodi na matumizi ya serikali. Hizi ni nguvu mbili zinazoweza ama kusukuma taifa mbele, au kuliingiza katika matatizo ya kifedha.

Makala yalionesha namna usimamizi mbaya katika maeneo hayo muhimu unavyoweza kusababisha upungufu katika bajeti, matumizi mabaya na hata kupoteza imani ya umma.

Ukweli usiopingika ni kuwa, usimamizi mbovu wa fedha unazifanya nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, kurudi nyuma kimaendeleo. Leo makala yanazama ndani zaidi kutazama changamoto halisi zinazozuia mabadiliko kutokea. Hapa
swali kubwa ni je, tunaweza kuvunja mzunguko huo, au tumekwama kwa kurudia makosa yale yale?

Hapa, tunajikita katika changamoto kubwa zinazoikabili serikal katika kuleta mabadiliko ya maana ya kifedha.
Tutaangalia vizuizi vya serikali kufikia ukuaji thabiti na endelevu wa uchumi kuanzia katika msukumo wa kisiasa na mifumo iliyopitwa na wakati, hadi taasisi dhaifu na deni linalokua.

Kwa muda mrefu masuala haya yamekuwa yakirudisha nyuma mataifa ya Afrika na sasa tunajiuliza swali kuwa, je, maboresho ya kweli kifedha yatapatikana, au mifumo hii imevunjwa kiasi cha kutoweza kurekebishwa!

Ili kufikia mabadiliko yenye tija katika sera za kodi na matumizi ya serikali, inahitajika mbinu ya kutumia awamu iliyopangwa na kuratibiwa vizuri. Hii itaharakisha uboreshaji huku ikiweka mazingira ya uendelevu wa muda mrefu wa fedha.

Meneja wa Kodi wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Geita (GGML), Godvictor Lyimo akitoa mapendekezo kuhusumfumo wa kodi nchini mbele ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi katika mkutano wa hivi karibuni mkoani Geita.(Picha na Samwel Mwalongo)

Mkakati uliopangwa na kuratibiwa sawia hupunguza upinzani wa kisiasa, kuchochea ulipaji kodi na kuimarisha uhimilivu wa uchumi.

Hapa, makala inawasilisha mfumo unaoelezea mchakato wa maboresho unaoendelea kwa kuanza na hatua zenye athari kubwa zinazoweza kufikiwa na kubadilika kuelekea mabadiliko ya kina kimuundo yanayohitaji ahadi thabiti za kitaasisi na kisheria. Kwa kufanya hivyo, inaweka njia bora kwa vizazi vijavyo.

Maboresho ya haraka
Kwa mujibu wa wachambuzi mbalimbali akiwemo Dlamini Amogelang ambaye ni mwanauchumi aliyepo Pretoria nchini Afrika Kusini, awamu ya kwanza ya maboreshoya kodi inapaswa kulenga hasa katika kuimarisha uwazi, kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kujenga upya imani ya umma katika usimamizi wa fedha kwa kati ya miezi 6 hadi 12 ya kwanza ya utekelezaji.

Amogelang anazungumzia mageuzi ya kidijiti yanayotoa athari chanya na kwa gharama nafuu huku akili mnemba (AI) na kujifunza kwa mashine vikiwa na nafasi kubwa katika kuleta mapinduzi katika usimamizi wa kodi.

Kimsingi, teknolojia hizi zinaweza kugundua mifumo ya ukwepaji kodi, zinaweza kutambua walipa kodi wasiotekeleza wajibu wao wa kulipa kodi na kuchochea ufanisi katika ukaguzi. Hapa, teknolojia inapaswa kutumika kufuatilia matumizi ya umma na kuhakikisha fedha za bajeti zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Amogelang anataja mafanikio ya mfumo wa serikali mtandao (e-Government) wa Estonia ambao umeongeza ufanisi wa kiusimamizi na kupunguza ufisadi katika sekta ya umma kwa zaidi ya asilimia 30 kupitia ufuatiliaji wa moja kwa moja wa kidijiti wa miamala ya fedha.

Huo umethibitika kuwa bora na unaoleta mabadiliko. Mchumi katika Ofisi ya Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania (jina linahifadhiwa), anasema ni muhimu kuimarisha mifumo huru ya usimamizi ili kuhakikisha kuna uwajibikaji wa fedha.

Akitumia mfano wa mbinu ya Shirika la Misaada la Marekani (USAID), anasisitiza taasisi kuu za ukaguzi kuwa na mamlaka kamili ya kufanya ukaguzi kwa wakati sahihi katika matumizi ya wakati halisi kuwa wa lazima kwa
mashirika yote ya serikali.

Caleb Ngozi ambaye ni mtaalamu wa uchumi aliyepo Arusha, anaunga mkono kauli hiyo akisisitiza kuwapo ufanisi
katika upangaji shirikishi wa bajeti kuwezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika uamuzi wa ugawaji wa bajeti.

Akirejea uzoefu wa nchini Brazili, anasema mbinu hiyo ilipunguza asilimia 20 ya matumizi yanayohusiana na rushwa huku ikiongeza imani ya umma katika matumizi ya serikali. Maboresho hayo si tu kwamba yatapunguza uwepo wa usimamizi mbaya wa kifedha, bali pia yataimarisha uhalali wa ukusanyaji wa kodi na kuhakikisha kuna mfumo wa fedha ulio wazi zaidi na unaowajibika.

Hamisi Aweso wa Mwanza, anasema kuongeza ukusanyaji wa kodi bila kuongeza viwango vya kodi kunaweza kuleta faida kubwa ya mapato. Anasisitiza urahisishaji kanuni za kodi na kuondoa vikwazo vya ukiritimba ili kuchochea ulipaji kodi hususani miongoni mwa biashara (mashirika) ndogo na za kati.

Aweso anaitazama nchi ya Rwanda kama mfano wa mafanikio. Anasema ujumuishaji wa uwekaji kodi kidijiti na
usajili wa kodi na mifumo ya vitambulisho vya kitaifa ulichochea ulipaji kodi kutoka asilimia 53 hadi 78 katika kipindi cha miaka mitatu pekee.

Anasema kupanua juhudi hizi kupitia wakala wa ukusanya mapato si tu kwamba kutasaidia kuziba ya mapengo ya kodi yaliyopo, bali pia kutapunguza gharama za usimamizi na hatimaye kuimarisha mfumo mzima wa kodi.

Maboresho ya muda wa kati
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wabunge mkoani Dodoma anasema baada ya kufanyika
maboresho ya awali ya uwazi na ufanisi kubainika, changamoto kubwa itakuwa kurekebisha matumizi ya serikali na kuboresha mgawanyo wa mapato katika kipindi muhimu cha miaka 1-3 baada ya utekelezaji.

Chini ya mtindo huu, wizara na mashirika yasingefanya kazi pamoja na maombi ya bajeti ya wazi, lakini yangehitajika kuthibitisha kila matumizi kupitia viashiria wazi vya utendaji vilivyo wazi vinavyotokana
na data inatathmini gharama na faida inayoonekana katika uwekezaji.

Akitumia Singapore kama mfano, anasema njia hiyo imethibitishwa kuwa muhimu kudumisha si tu ufanisi wa kifedha, bali pia uwiano wa chini wa deni kwa Pato la Taifa unaolifanya taifa kuwa kama kiongozi wa kimataifa katika uendelevu wa fedha za umma.

Mbunge huyo anasema Tanzania inapaswa kupitisha mwongozo huo kama inataka kuvunja mzunguko wa uzembe
na kuunda serikali inayowajibika zaidi. Mmoja wa wajumbe wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania anasisitiza haja ya maboresho ya kodi kwa sekta mahususi kukuza uchumi na kuchochea usawa.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo, serikali inapaswa kupunguza mzigo wa kodi kwa sekta zinazoajiri zaidi kama vile
viwanda, kilimo na teknolojia. Kwamba, serikali ichukue hatua makini katika sekta zenye michango midogo ya kodi
zikiwamo sekta za uchimbaji na huduma za kidijiti.

Mwenzake anajikita katika sera za kimkakati za kodi za mashirika za Ireland kama mfano bora wa namna utozaji kodi kusudiwa, unavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi. Kwa kutoa viwango shindani vya kodi kwa mashirika
ya kimataifa huku ikihakikisha kuna ulipaji kodi stahiki, mapato ya kodi ya Ireland ‘yalipaa’ kutoka Euro bilioni 4
mwaka 2010, hadi Euro bilini 22 bilioni mwaka 2022.

Hii inathibitisha umuhimu wa kipekee wa kuoanisha sera za kodi na vipaumbele vya uchumi vya taifa kwa ajili ya
ukuaji endelevu. Mfanyakazi wa Benki ya Dunia ambaye jina lake halikupatikana mara moja anabainisha jambo muhimu.

Anasema ili kulinda afya ya kifedha ya Tanzania kwa muda mrefu, serikali inapaswa kutekeleza sheria thabiti za
uwajibikaji wa kifedha na hatua za kudhibiti madeni. Wazo la kuweka kanuni za ukomo wa nakisi (upungufu) wa bajeti kuwa sheria, masharti ya mapitio ya matumizi ya kielektroniki pamoja na sera rekebishi za fedha kunapotokea
upungufu unaozidi viwango vilivyowekwa, linaweza kuleta mabadiliko.

Si tu kwamba hatua hizo zitaimarisha nidhamu ya fedha, bali pia zitaimarisha imani ya umma na kukuza utulivu wa
uchumi nchini. Hata hivyo, vikwazo vinavyowezekana vya kisiasa hususani umuhimu wa kupunguza matumizi yasiyofahamika na watu wengi ni mambo yasiyopaswa kupuuzwa.

Mazungumzo yaliegemea zaidi katika sera ya Ujerumani inayosifiwa kama mwanga wa nidhamu ya fedha. Kwa kutunza deni lake la kitaifa chini ya asilimia 70 ya Pato la Taifa, tofauti kabisa na zaidi ya asilimia 100 katika nchi
jirani za Ufaransa na Uingereza, Ujerumani inatoa somo kubwa katika ufadhili endelevu wa umma.

Kimsingi kupitisha mfumo kama huo kunaweza kuvunja mzunguko wa ukopaji usio endelevu na kuleta utulivu wa nchi kwa vizazi vijavyo.

Maboresho ya kimuundo na kitaasisi
Awamu ya mwisho na hata zaidi ya maboresho inahusu kuoanisha sera za kodi na matumizi pamoja na malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya taifa. Mchakato huo unaweza kufanyiwa tathmini kati ya miaka 3 na 10 ya mzunguko wa utekelezaji.

Mchumi na mpanga mikakati ya mashirika anayeishi Nairobi Kenya, Andrei Mikhail anasema badala ya kuingizwa katika mgao wa jumla wa bajeti, mapato ya kodi yanapaswa kutengwa kwa ajili ya huduma muhimu za umma zikiwamo za afya, elimu na miundombinu.

Kwa mujibu wa Mikhail, Tanzania haina budi kuanzisha mamlaka ya kikatiba itakayoweka viwango vya chini vya
matumizi kwa sekta muhimu na kuhakikisha kuna uwekezaji endelevu katika rasilimali watu sambamba na ushindani wa muda mrefu wa kiuchumi.

Kutokana na mafanikio yaliyopatikana Sweden ambapo kodi ya juu inahusishwa moja kwa moja na huduma bora za
kijamii, Mikhail anasema mbinu hii imeipa Sweden asilimia 78 ya uidhinishaji wa viwango vya ukadiriaji wa umma kwa sera zake za kifedha ikionesha faida za mbinu kama hiyo.

Mtendaji Mkuu wa The Morocco Inter-Professional Retirement (CIMR), anasisitiza umuhimu wa maboresho ya kina
katika pensheni na mishahara ya umma ili kuhakikisha kuna uendelevu wa fedha wa muda mrefu. Anasema, “Serikali nyingi barani Afrika, zinakabiliwa na majukumu ya pensheni yasiyo endelevu kutokana na ongezeko la wazee na kupungua kwa ushiriki wa nguvu kazi.”

Akitoa mfano wa utafiti, anasema kuhama kutoka katika mifumo ya pensheni ya jadi iliyoainishwa ya faida hadi
mifumo inayotegemea michango kunaweza kupunguza shinikizo la kifedha huku ikiendelea kutoa msaada wa kutosha kwa wastaafu.

Anazungumzia maboresho ya pensheni nchini Italia yaliyoongeza umri wa kustaafu hadi miaka 67 kama mfano wa namna hatua kama hizo zinavyoweza kuleta utulivu wa matumizi ya pensheni ambayo awali yalitumia zaidi ya asilimia 16 ya Pato la Taifa.

Katika majadiliano hayo, anasema uchumi unaokabiliwa na changamoto sawa za idadi ya watu unapaswa kuzingatia kupitisha maboresho sawa ili kulinda utulivu wa kifedha. Anaungana na wataalamu wengine kusisitiza haja ya maboresho ya mishahara katika sekta ya umma ili kuzuia matumizi makubwa ya mishahara na kuhakikisha fedha za
kutosha zinapatikana kwa ajili ya huduma muhimu badala ya gharama kubwa za mishahara.

Mhitimu wa Shule ya Biashara ya McDonough katika Chuo Kikuu cha Georgetown chenye makao yake makuu nchini
Ghana, Manish Ishaan anasisitiza haja ya haraka kwa Tanzania kuweka kipaumbele katika mseto wa kiuchumi na utulivu wa mapato ili kupunguza utegemezi wake katika vyanzo tete vya mapato hasa mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Anasema kwa sasa usimamizi unapaswa kuwekeza mapato yoyote ya ziada ya kodi katika mipango iliyoundwa kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa nchi kwa muda mrefu. Kutokana na utafiti huu, Ishaan anazungumzia mafanikio ya Mfuko Mkuu wa Norway, wenye thamani ya Dola trilioni 1.4 unaotumika kama ngao (kinga) dhidi ya
mabadiliko katika mapato ya mafuta.

Kwa kubadili vyanzo mbalimbali vya mapato na kuanzisha mifuko kama hiyo, nchi zenye rasilimali lakini ziko hatarini kiuchumi kama Tanzania zinaweza kujilinda dhidi ya migogoro ya kibajeti bei za bidhaa zinapoyumba na kuhakikisha matumizi ya serikali ni utulivu naendelevu.

Mwelekeo wa maboresho
Kufikia maboresho endelevu ya kodi na matumizi kunahitaji mbinu za kuwianisha faida za haraka za mapato na utulivu wa muda mrefu wa uchumi.

Serikali inapaswa kuanza na hatua za haraka, zenye matokeo makubwa na kuweka uangalizi ulioboreshwa wa kidijiti kabla ya kuendelea na mabadiliko ya kimuundo katika upangaji wa bajeti na kupatanisha sera ya kodi na usimamizi
wa madeni.

Maboresho yenye changamoto na hatimaye kuleta mabadiliko yanahusisha marekebisho ya kitaasisi, uendelevu wa pensheni na uchumi mseto wa kiuchumi unaohitaji utashi thabiti wa kisiasa na kujitolea kwa muda mrefu.

Mkakati huu wa awamu hutoa mwelekeo wa kitaalamu kwa watunga sera kuhakikisha mifumo ya fedha inakuwa wazi, yenye ufanisi na inayowiana na malengo ya maendeleo ya kitaifa.Utekelezaji wenye mafanikio unategemea
ujumuishaji wa teknolojia za kidijiti, mifumo ya kisheria inayotekeleza na kuzingatia nidhamu ya fedha na ushirikiano endelevu wa umma.

Kwa kufuata mchakato huu wa maboresho, serikali zinaweza kuunda mifumo ya kodi na matumizi inayokuza ustahimilivu wa kiuchumi, ukuaji wa usawa na uendelevu wa kifedha wa muda mrefu.

Hitimisho
Maboresho ya kodi na matumizi si mada ya mjadala usioisha, bali yanahitaji hatua madhubuti. Nchi kama Estonia,
Singapore na Ujerumani ni uthibitisho kwamba kuoanisha sera za kodi na matumizi wajibifu si tu kwamba kunawezekana, bali ni muhimu.

Kupitia uvumbuzi wa kidijiti, nidhamu katika fedha pamoja na mifumo ya kodi iliyopangwa sawia, mataifa haya yameweka alama mataifa mengine kufuata. Kwa watunga sera, njia ya kusonga mbele iko wazi kwamba, anza kwa kuboresha mifumo ya kodi na kufanya ukaguzi makini kabla ya kuendelea na maboresho ya kina ya kimuundo kama
kuondoa ruzuku zisizo na tija na kuunda upya makundi ya kodi.

Ujenzi wa taasisi imara na kukuza uangalizi wa umma ni mambo yasiyohitaji mjadala kuendeleza juhudi hizi. Kimsingi, wajibu wa raia, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia hauwezi kupitiwa kupita kiasi. Hivyo, ni wakati sasa kudai uwazi, kutetea utozaji kodi wa haki na kuweka msukumo wa kuwepo kwa bajeti shirikishi zinazotoa
kipaumbele katika ukuaji wa muda mrefu wa taifa.

Enzi ya hatua nusu lazima imalizike, maboresho ya haraka yanayoongozwa na data yanaweza kuepusha mizozo ya kifedha katika siku zijazo.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button