Samia atabiri mema nishati safi ya kupikia

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na kasi kubwa ya utekelezaji wa mkakati wa kusambaza nishati safi ya kupikia, nchi itafikia lengo lake kabla ya 2030.

Ameeleza hayo kwenye Uwanja wa CCM Jitegemee wilayani Muheza baada ya kukabidhi mitungi ya gesi ya ruzuku kwa wananchi wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Tanga wakati wa mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.

Alisema kwa sasa utekelezaji wa mkakati huo upo chini ya asilimia 10, lakini anao uhakika kwamba kabla ya kufikia mwaka 2030, lengo la kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania litakuwa limefikiwa kutokana na kasi kubwa ya utekelezaji.

“Tulisema asilimia 80 ya watu wetu ikifika 2030 wawe na nishati safi ya kupikia na kwa sasa tupo chini ya asilimia 10, lakini kwa kasi tunayoendelea nayo nina hakika kabla ya kufika 2030 tutakuwa tumefikia lengo tulilojiwekea
kwenye mkakati wetu… hilo nina hakika,” alieleza Rais Samia.

Alisema juhudi zimeendelea kufanyika kulifikia lengo hilo ikiwamo usambazaji wa mitungi, upanuzi wa huduma kwenye vijiji ambako zipo kampuni zinazofungua maeneo yatakayotumika kubadilisha mitungi pindi gesi zitakapowaishia watumiaji.

“Nimeona pia, ubunifu wa teknolojia mbalimbali ambazo zinakwenda kubana matumizi katika kutumia nishati safi ya kupikia, tunafanya hivi ili kulinda mazingira na afya za wapishi, wengi wao wakiwa akina mama,” alifafanua.

Tofauti na gesi, Rais Samia alisema wataalamu wamebuni mkaa wa kupikia unaotokana na makaa ya mawe ambayo
nayo yatatumika kama nishati safi kuongeza nguvu kwenye gesi ambayo kwa sehemu kubwa ndiyo inayotumika kama nishati safi.

“Tumeanza kutoa ruzuku kwa wote wenye miradi ya gesi ambao wanachakata kuifanya gesi iwe nishati, lakini ndani ya mkakati wa nishati safi ya kupikia tumeendelea kutoa ruzuku kwa majiko ya gesi ambapo serikali inachukua asilimia 50 na wanunuzi tunataka watoe asilimia 50.

Hii ni kutokana na Sheria ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inayosambaza umeme vijijini, tumetumia sheria
hiyohiyo kutoa ruzuku hiyo,” alisema Rais Samia.

Aliongeza: “Tunaposambaza umeme vijijini tunataka umeme huo uwe zaidi ya kuwasha taa na kuchaji simu, ndiyo maana tunatoa ruzuku hizi na tumetoa ruzuku hata kwenye majiko ya umeme.

Nimepita banda moja wamesema haya majiko ni oda maalumu ya ruzuku tunayatengeneza yaende vijijini na
tunayauza kwa bei ya ruzuku ili umeme unaokwenda vijijini utumike pia kwenye kupikia”.

Alisema katika mazingira ya sasa kama matumizi ya kuni na mkaa yakiendelea kufanyika kama nishati kuu ya kupikia, ni dhahiri nchi itakumbana na majanga yatakayokausha vyanzo vya maji na upatikanaji wa chakula utakuwa wa shida.

Akizungumzia changamoto alizoziwasilisha kwake Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma, Rais Samia alisema kuhusu kupatikana kwa soko la machungwa Muheza, kinachotakiwa ni uwepo wa kiwanda.

Amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian na Waziri wa Viwanda, Dk Selemani Jafo kurahisisha
mchakato wa mwekezaji aliyepatikana kuweka kiwanda ili wakulima wawe na kiwanda na soko la uhakika la kuuza machungwa yao.

“Pia lingine alilosema ni kwamba kata mbili hazina sekondari, nilidhani kwamba tungefanya jambo hili kabla ya kuingia kwenye uchaguzi lakini kwa hapa tulipofika na mwaka huu ulivyo hizi sekondari mbili zitajengwa mapema baada ya uchaguzi,” alisema Rais Samia.

Aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kujenga
barabara kuelekea katika Kijiji cha Magoroto ambako mbunge amejenga shule.

“Jambo jingine ni barabara ya lami Amani-Muheza, barabara hii tunaijua na tumeanza kujenga ni barabara ya kilometa 40 ambapo tumeweza kujenga kilometa 14 na kilometa zingine tatu zitajengwa mwaka huu,” alisema Rais Samia.

“Pia, lipo pendekezo la kujenga Barabara ya Muheza – Pangani na kwa sasa bado haijafanyiwa usanifu lakini
niwaahidi kwamba barabara hii tunakwenda kuiweka kwenye Ilani ya Uchaguzi inayoandikwa mwaka huu kwenda miaka mitano ijayo,” aliongeza Rais Samia ambaye ni mgombea urais wa CCM mwaka huu.

Kuhusu kutokuwepo kwa mashine ya kuchakata mkonge katika Shamba la Kibaranga alisema suala hilo analifahamu
na serikali iliagiza mashine hizo na zipo nchini na imeagiza zingine 10 na moja kati ya hizo itaenda Kibaranga.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button