Minziro: Tunawaheshimu Yanga, wasituchukulie poa

KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Felix Minziro, amesema timu yake inatambua changamoto ya kucheza dhidi ya timu kubwa kama Yanga, lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa upinzani mkali katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hizo leo.

Akizungumza kuelekea pambano hilo litakalochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Minziro amesema  presha ni jambo la kawaida unapokutana na timu yenye wachezaji bora na uzoefu mkubwa.

“Unapocheza na timu kubwa kama Yanga, lazima uwe na mpango mzuri wa mchezo. Tunafikiria jinsi ya kujipanga, kujilinda, na kutafuta mabao. Tumerekebisha makosa yetu katika safu ya ushambuliaji na ulinzi ili kuhakikisha tunatoa ushindani wa hali ya juu,” amesema Minziro.

Pia ameongeza kuwa Pamba Jiji imefanya mabadiliko makubwa na mashabiki wanapaswa kutegemea mchezo mzuri wenye ushindani.

“Tunawaheshimu Yanga kwa sababu wamewekeza vizuri, lakini sisi pia tumeimarika. Mashabiki wategemee kuona mechi kali na yenye ushindani,” amesema.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa, kwani Pamba Jiji itakuwa na faida ya kucheza nyumbani mbele ya mashabiki wao, huku Yanga ikisaka pointi muhimu kuendelea kuimarisha nafasi yake katika ligi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button