Kampeni ya Samia yapokea migogoro 3,912 mikoa sita

KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwenye mikoa ya Arusha, Mbeya, Mwanza, Lindi, Rukwa, Pwani imewafikia na kuwapatia elimu na msaada wa kisheria wananchi 565,198 huku migogoro 3,912 ikiwa imepokewa.

Taarifa ya Wizara ya Katiba na Sheria imeeleza kuwa kampeni hiyo ilifanyika kwa siku tisa kuanzia Februari 20 hadi Machi Mosi mwaka huu.

Migogoro iliyopokewa ni inayohusu ajira, ardhi, jinai, madai, matunzo ya watoto, mirathi, ndoa ukatili wa kijinsia na ipo katika hatua mbalimbali za kutatuliwa.

Akizungumza jana kuhusu wiki ya utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria inayoenda sambamba na shamrashamra za kuelekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, inayofanyika kitaifa jijini Arusha, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini alisema wananchi wanaohitaji huduma za kisheria ni wengi na sekta zote muhimu zipo kwenye kampeni hiyo.

Alisema malalamiko mengi yamejikita kwenye sekta ya ardhi. Aliwataka wataalamu kuungana na kutatua papo kwa hapo na kuwasikiliza wananchi kwa utulivu.

“Kwenye mikoa tuliyopita, wenye uhitaji ni wengi, hii fursa iliyotolewa na Rais Samia ambayo inatoa huduma bure imesaidia sana wananchi. Na kwa kutambua uzito huo, serikali imeajiri vijana wa maendeleo ya jamii zaidi ya 500 ili kazi hii inayofanywa iwe endelevu na si kusubiri wakati wa kampeni,” alisema.

Miongoni mwa migogoro iliyotatuliwa kwenye kampeni hiyo kwa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi ni wa majirani wawili uliodumu kwa miaka 12 na walikuwa wakigombea mnazi.

Timu ya wataalamu wa kutoa huduma ya msaada wa kisheria ilifika Mtaa wa Tunduru kwenye Kata ya Nachingwea na kutatua mgogoro kati ya Mariam Mponda na Habiba Mpoyo ulioanza 2013 ukihusu mnazi mmoja uliopo mpakani mwa makazi yao.

Habiba alikuwa akisisitiza kuwa mnazi huo ni mali yake na haupaswi kukatwa huku Mariam akidai unaharibu mabati ya nyumba yake akitaka ukatwe.

Kutokana na mvutano huo, wataalamu hao wa kisheria wa Mama Samia walisikiliza kwa kina na walipata suluhu ya pamoja kwa kuamua mnazi ukatwe ili kuepusha madhara zaidi na majirani hao kurejesha uhusiano wao.

Pamoja na hilo, timu hiyo ilifanikiwa kuwapatanisha wazazi wenza wa mtoto (jina limehifadhiwa) katika Kijiji cha Nammanga wilayani humo ambao walikuwa wana mgogoro wa muda mrefu ulioathiri ustawi wa mtoto wao.

Pia, katika Kijiji cha Dimbwe, kampeni hiyo imetatua mgogoro wa mpaka wa wanafamilia uliodumu kwa miaka tisa na kufanikiwa kuweka mipaka mipya na kupatanisha ndugu hao.

Kadhalika, katika Mkoa wa Mbeya, kampeni ilifanikiwa kuirejesha ndoa ambayo wanandoa walitengana miaka miwili iliyopita kati ya Eleneo Mbilinyi na Rebecca Ndidi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button