Watumishi Chato watakiwa kuondoa matabaka kazini

WATUMISHI wa taasisi tofauti ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Chato wametakiwa kuondoa matabaka ya kiutendaji baina yao ili kuimarisha mahusiano kazini na kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato, Thomas Dimme ametoa maelekezo hayo katika hafla ya watumishi wa halmashauri hiyo iliyofanyika kwa ajili ya kuukaribisha mwaka mpya wa utumishi 2025.

Dimme amesema mshikamano wa watumishi wa taasisi zote utasaidia siyo tu kuimarisha umoja lakini pia kuwasaidia wananchi kupata msaada wa haraka na huduma kwa urahisi kwenye ofisi zote za halmashauri.
“Jambo la mtumishi wa magereza, jambo la mtumishi wa ofisi ya mkuu wa wilaya, jambo la mtumishi wa halmashauri ni jambo letu sote,”
“Tunayo kauli mbiu yetu inayosema, watumishi Chato 2025 weledi, uadirifu, upendo, mshikamano twende tukaiishi kauli mbiu hii.

“Niwaombe tushike sana kauli mbiu hii, kuna uadirifu, kuna weledi, lakini kuna mshikamano na umoja, jambo la furaha na matatizo litakalojitokeza Chato tuwe pamoja tushirikiane, amesema Dimme.
Aidha Dimme amewataka wakuu wa Taasisi na waajiri wote kuhakikisha wanatoa muda na fursa ya kukutana na watumishi ili kusikiliza kero na kuzitatua kwa wakati waweze kuendelea na majukumu yao.
“Tunayo fursa kubwa ya kuhakikisha watumishi tunaowasimamia, wanatendewa haki, wanasikilizwa, ili waweze kuwahudumia wananchi wetu wa wilaya ya Chato”, amesisitiza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chato, Mandia Kihiyo amesema mpaka Februari 28, 2025 halmashauri ina takribani watumishi 3600 ambao wapo katika ngazi mbalimbali za kiutumishi.

Amesema maisha ya utumishi wa umma kuanzia kuajiriwa mpaka kustaafu ni marefu hivo ni lazima kuwe na mazingira bora ya watumishi kuwa na furaha, amani na upendo ili wafanye kazi yao bila kikwazo.
Mbunge wa Jimbo la Chato, Dk Medard Kalemani amesema hafla za watumishi ni chachu kubwa katika kuhamasisha utendaji hivo aliahidi kufadhili hafla zijazo ili watumishi wapate nafasi ya kufurahi.
Awali Kaimu Ofisa Michezo wilaya ya Chato, Mwalimu Mataba Abel amesema hafla ya watumishi ilitanguliwa na bonanza la michezo mbalimbali kwa kushirikisha taasisi 12 za halmashauri.
“Huu utakuwa ni mwendelezo kwa ajili ya kuhamasisha uhusiano ndani ya kazi, lakini urafiki na udugu kwa watumishi waliopo ndani ya halmashauri ya wilaya ya Chato, amesema Abel.



