Mmesikia haya ya Nicole?

UMDHANIAE Siye, Kumbe Ndiye! Usemi huu unadhihirika katika sakata linalomhusisha msanii wa maigizo na mfanyabiashara Nicole Joyberry, ambaye kwa sasa anakabiliwa na tuhuma za kujihusisha na utapeli kupitia mitandao ya kijamii. Umaarufu wake uliwafanya watu wengi kumuamini, lakini sasa anatuhumiwa kuwatapeli wafuasi wake kwa njia ya ulaghai wa kifedha.
Kutokana na tuhuma hizo, zaidi ya wananchi 20 wamejitokeza na kufika katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam ili kutoa malalamiko yao. Wanasema wamepoteza fedha zao wakiamini kuwa wanashiriki mpango halali, lakini baadaye wakagundua wameingizwa kwenye mtego wa kitapeli unaodaiwa kuendeshwa na msanii huyo.
Kwa mujibu wa malalamiko yao, Nicole alitumia mitandao yake ya kijamii, hasa Instagram, kuwashawishi watu kujiunga na mchezo huo. Umaarufu wake ulimfanya wengi waamini kuwa ni fursa halali ya kupata faida, jambo lililowafanya kushiriki kwa wingi.
Hata hivyo, wananchi hao wanasema baada ya kujiunga, hawakupata mafanikio yoyote. Walipojaribu kuulizia kuhusu hatma ya fedha zao, Nicole alikwepa kutoa ushirikiano au maelezo yoyote yanayoeleweka.
Mmoja wa wahanga anayedai zaidi ya Sh milioni 26 amesema: “Utapeli alioufanya huyu alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba ana makundi ‘group’ ya michezo, akatengeneza ‘magrupu’ kama manne, na baada ya kufuatilia tukagundua kwamba za kwanza za juu ni zake yeye, ni watu anaowajua yeye, kwamba hapa tumetapeliwa, na simu akawa anablock mara hapokei simu ndio tukagundua kuwa tumetapeliwa”
Muhanga mwingine (hakutaja jina) anayedai milioni 7 amesema “Nilipewa taarifa na mshikaji wangu akaniambia Nicole hana shida, ‘round’ ya pili alitumia nguvu kubwa sana kushawishi watu, muda ambao mimi nilitakiwa kupewa fedha alikuwa akinizungusha sana na baada ya kufuatilia tukagundua kwamba amewadhulumu watu wengi”
Kutokana na malalamiko hayo, inaripotiwa kuwa tayari Nicole amekamatwa na yuko chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Hatua hii imekuja baada ya wananchi hao kufikisha kesi yao kwa vyombo vya sheria wakitaka haki itendeke. Hata hivyo wahanga hao wamewataka watu kuacha kuwaamini wasanii kwa kuwa sio kila msanii ni muaminifu.