Yanga: ‘Derby’ ipo palepale

Uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza kuwa mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopangwa kuchezwa leo usiku dhidi ya Simba upo palepale na hakuna mabadiliko yoyote.

Taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine imesema timu hiyo kama wenyeji wa mchezo, inaamini taratibu zote za mchezo kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za Ligi Kuu ziko sawa maandalizi yote yako tayari.

“Uongozi wa Young Africans SC utapeleka timu uwanja wa Benjamin Mkapa kama inavyoelekezwa kwenye kanuni, na hatutakuwa tayari kucheza mchezo huu siku nyingine tofauti na leo,” imesema taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo Yanga imewaalika uwanjani wanachama, mashabiki, wapenzi wa klabu hiyo na wadau wengine waliosafiri kutoka mikoani, nchi za jirani na sehemu mbalimbali duniani kote kwenda kushuhudia mchezo huo mkubwa barani Afrika.

Usiku wa kuamkia leo Menejiment ya klabu ya Simba ilitoa taarifa ya kutopeleka timu uwanjani ikidai kusikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana dhidi ya timu hiyo kuelekea mchezo huo.

“Kwa mujibu wa Kanuni 17(45) ya Kanuni za Ligi Kuu Bara, Timu Mgeni ina haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Kwa makusudi Simba imenyimwa haki hiyo licha ya kufika uwanjani katika muda husika,”ilisema taarifa ya Simba.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button