Samia aonya usumbufu kwa wawekezaji nchini

RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya viongozi wanaosumbua wawekezaji.

Akifungua Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma, Rais Samia ameagiza halmashauri zihakikishe kuwa maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji yanatumika kama ilivyokusudiwa.

Ameeleza kushangazwa na vitendo vya kuwanyima wawekezaji ardhi wakati serikali inafanya juhudi kushawishi na kuleta wawekezaji nchini.

Amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa halmashauri kujenga mazingira ya kupata rushwa kutoka kwa wawekezaji wa ndani kama sharti la kupata ardhi ya kuwekeza.

“Hakuna sababu kwa wawekezaji kusumbuliwa kwa sababu serikali inatumia nguvu kubwa kuwavutia wawekezaji kuja nchini kuwekeza kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Rais Samia.

Kwa upande wa wawekezaji wanaokiuka taratibu na makubaliano ya uwekezaji, Rais Samia alizitaka halmashauri zote zifuate utawala wa sheria katika kuwachukulia hatua wawekezaji wakorofi ili kuepusha serikali kulipa fedha nyingi pale wawekezaji hao wanaposhinda kesi zao mahakamani.

Aidha, alizitaka halmashauri nchini kujiepusha kutumia mabavu katika kushughulika na wawekezaji na pale inapotokea zihakikishe zinamshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kujenga mazingira mazuri ya maelewano kuepusha gharama kubwa inayoweza kuikabili serikali baadaye.

Ameziagiza halmashauri zote kusimama imara na kuwa makini katika ukusanyaji wa mapato pamoja na matumizi yake ili mapato yote yatumike kwa njia sahihi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa na wakurugenzi wote wa halmashauri kuwa macho na viongozi wanaobuni njia ya kufuja fedha za serikali na kuisababishia hasara.

“Kama mmewabaini hawa watu (walioghushi risiti), tafadhali sana lile jicho lako la huruma hapa hapana, hapa
hapana,” alionya Rais Samia.

Alisema wengine wanatoa risiti za udanganyifu kwa maana wanakusanya mapato huku wakitoa risiti zisizo halisi na kwamba kama watu hao wamegundulika, hatakuwa na ‘mswalie mtume’ na kwamba kama waziri Mchengerwa atashindwa kuwachukulia hatua basi atachukuliwa hatua yeye mwenyewe pamoja na wabadhirifu hao.

Aliitaka Tamisemi kwa pamoja na halmashauri kujipanga kuzuia wizi huo na kuhakikisha hakuna halmashauri inayoweza kufanya ubadhirifu wa fedha za serikali.

Ili halmashauri ziwe na mapato ya kutosha, aliwaagiza wakurugenzi kote nchini kubuni vyanzo vipya vya mapato katika miji midogo pamoja na majiji.

Katika kuzuia wizi wa mapato ya serikali, alizishauri halmashauri kusimamia sheria na sheria ndogo akibainisha kuwa ‘uchafu mwingi’ unaojitokeza katika halmashauri unasababishwa na kutosimamiwa kwa sheria na sheria ndogo.

Rais Samia alitolea mfano katika ujenzi kuwa sheria inawataka watu wote wanaotaka kujenga kuwa na vibali, na kueleza kuwa asilimia kubwa ya halmashauri hazifuatilii vibali hivyo kuwa kilichojengwa ndio kilichoruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

Akitolea mfano wa Kariakoo katika Manispaa ya Ilala, Rais Samia alisema baadhi ya wamiliki wa majengo hawakufuata matakwa ya vibali vyao vya ujenzi kwa sababu wengi wao wanajenga jengo lake na kuongeza ‘lumbesa’
juu yake.

Kwa upande wa halmashauri zilizokuwa na matumizi mazuri ya sehemu ya mapato yake, Rais Samia alieleza kufurahishwa na halmashauri za Ludewa, Tanganyika na Kwimba kutokana na kuwa na ubunifu mzuri katika matumizi ya mapato.

Mbali na hayo, alitoa maelekezo mahususi kwa wakurugenzi na halmashauri zao juu ya kuwahudumia ipasavyo wananchi kwa sababu hao ndio waajiri wao.

Amewaagiza wakurugenzi kwenda kuitambua na kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao ili wananchi wapate haki yao, huku akiwakumbusha kuhakikisha hawawi sehemu ya migogoro hiyo kwa sababu watasababisha utatuzi wake kuwa mgumu.

Vilevile, Rais Samia aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa mipango yao katika halmashauri zao inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.

Kuhusu viongozi katika halmashauri wenye tamaa ya kutangaza nia katika Uchaguzi Mkuu ujao, aliwakumbusha kuwa kiongozi yeyote mwenye nia hiyo ahakikishe anatoa taarifa mapema ili mipango ya kutafuta mrithi wa nafasi yake ifanywe mapema.

Alionya watakaoenda kugombea bila kutoa taarifa kwamba ikiwa watakosa nafasi hizo watakuwa wamejiondoa katika utumishi, na kwa atakayetoa taarifa kisha akashindwa, serikali itapima uwezo wake ili kama unaridhisha atarudishwa katika nafasi yake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button