Tuiamini serikali usimamizi nishati ya umeme

KATIKA moja ya mambo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ni usimamizi thabiti katika sekta ndogo ya umeme ambao umeiwezesha nchi kuwa na umeme wa uhakika.
Katika miaka michache iliyopita, nchi ilikuwa na kelele nyingi kuhusu upatikanaji wa umeme katika maeneo mengi, lakini leo hii vilio hivyo vimefutika.
Leo hii serikali inachofanya sasa ni kupeleka umeme katika vitongoji baada ya kukamilisha kupeleka umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara. Na hii imefanyika kwa kuhakikisha mikoa ambayo ilikuwa haijaungwa na Gridi ya Taifa ya Umeme kupata huduma hiyo.
Mikoa kama Kagera na Kigoma hivi sasa inajivunia kutumia umeme wa gridi na kuachana na umeme wa majenereta.
Kama hiyo haitoshi, serikali imekamilisha mradi mkubwa wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji ambao muda si mrefu utazinduliwa.
Takribani megawati zote 2,115 zinazozalishwa hapo, muda si mrefu zitaingia katika gridi.
Mbali na mradi huo, serikali pia inaendelea na ujenzi wa miradi mingine ya umeme kwa njia mbalimbali ikiwamo ya maji, gesi na upepo, kiasi kwamba Tanzania itaendelea kuwa na umeme wa ziada na kuiwezesha kuuza nje ya nchi.
Ndio maana serikali imetoa ufafanuzi kuhusu kununua umeme kutoka nje ya nchi kwa ajili ya baadhi ya mikoa ya Kaskazini mwa nchi, ikieleza kuwa kununua na kuuziana umeme kwa nchi si jambo geni na Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikiununua Uganda kwa ajili ya Mkoa wa Kagera, nchini Zambia kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa na Kenya kwa baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga hususani yaliyoko mpakani.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, pia ununuzi wa umeme kutoka nchi jirani haumaanishi kwamba nchi ipo katika changamoto ya upungufu wa nishati hiyo kwa kuwa mpaka sasa Tanzania inazalisha umeme wa kutosha ambao ni takribani megawati 3,796.
Amesema uamuzi huo una faida kwa pande zote mbili kwa kuwa njia itakayotumiwa kununua umeme nchini Ethiopia ndiyo itatumika kuuza kwa nchi zenye uhitaji.
Kwa msingi huo, sisi tunaona kwamba taifa halina sababu ya kuwa na hofu inapoelezwa kwamba nchi itanunua umeme kutoka nje kwa sababu hali hiyo ni ya kawaida, na imekuwa ikifanyika hivyo kwa muda mrefu, na kwa sababu za kitaalamu.
Hivyo hata hili la sasa la kununua umeme kutoka Ethiopia lina faida na hasa ikikumbukwa kwamba kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda Zambia na kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kwa nchi kuuza umeme kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
Tuendelee kuiunga mkono serikali katika utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo ambayo tayari manufaa yake yameonekana, kwani sasa vijijini maisha yamebadilika baada ya umeme kufikishwa, na uchumi wa wananchi umebadilika.
Sasa hata vijana kukimbilia mjini kumeanza kuwa ni jambo lisilowezekana tena.



