Serikali yalihakikishia bunge kutafuta fedha miradi ya mazingira
SERIKALI imelieleza Bunge itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya hifadhi ya mazingira.
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema hayo Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Khamis alisema lengo la miradi ya hifadhi ya mazingira ni kuhakikisha Ofisi ya Makamu wa Rais inachangia katika mpango wa maendeleo wa taifa na ukuaji wa uchumi endelevu.
Alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025 miradi ya maendeleo ya hifadhi ya mazingira inayotekelezwa na kusimamiwa na ofisi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kuta katika fukwe za Mikindani- Mtwara na Sipwese- Pemba, mradi wa kuboresha eneo la Bwawa la kuhifadhi maji ya mvua la Swaswa-Mnarani.
Alitaja miradi mingine ni wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame ya Tanzania, mradi wa usimamizi jumuishi wa mifumo ikolojia, mradi wa urejeshwaji endelevu wa mazingira na hifadhi ya bayonuai Tanzania.
Khamis aliitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na wa kuandaa mkakati na mpangokazi wa taifa wa kuhifadhi bayonuai, mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia vijijini na mradi wa kujenga ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi mkoani Kigoma.
Alisema jamii zimewezesha utekelezaji wa shughuli mbadala za kiuchumi na rafiki kwa mazingira ikiwemo mipango ya kisasa ya ufugaji endelevu, uendelezaji wa mashamba darasa ya malisho, ujenzi wa skimu za umwagiliaji na mipango ya kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Khamis aliwaeleza wabunge kuwa miradi hiyo inatekelezwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuna tija katika ukuaji wa maisha na ustawi wa huduma za kijamii na kiuchumi kupitia uhifadhi endelevu wa mazingira.
Awali, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga aliipongeza ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa miradi hiyo.
Kamati hiyo inatarajia kutembelea miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ukiwemo wa kurejesha ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula.



