Wapelelezi wafundwa mbinu mpya makosa ya uhalifu

DODOMA: WAKUU wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mikoa na Vikosi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wametakiwa kutumia mbinu mpya katika upelelezi wa makosa ya uhalifu wa kifedha ili kuimarisha usalama wa nchi na kudhibiti uhalifu huo kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Ramadhan Kingai, ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo maalum ya upelelezi wa makosa ya kifedha kwa Wakuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mikoa (RCO’s) na Vikosi (DCO’s) yanayofanyika jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, DCI Kingai amesema kuwa RCO’s na DCO’s ni nguzo muhimu katika kudhibiti makosa ya kifedha, na mafanikio katika kesi za uhalifu huo yanategemea upelelezi wa kina unaozingatia mbinu za kisasa.
“Mafunzo haya ni nyenzo muhimu za kuwaimarisha katika utendaji kazi. Tumieni fursa hii kujifunza mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu wa makosa ya kifedha ili muweze kusimamia vyema wapelelezi walioko mikoani katika kukusanya ushahidi na kuwabaini wahusika wa uhalifu huu,” alisema DCI Kingai.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Saleh Ambika, alisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu, hasa katika kipindi hiki ambacho Jeshi la Polisi linaendelea kufanya maboresho, ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika upelelezi wa makosa ya jinai.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Makosa dhidi ya Fedha (FCU), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Hapiness Laizer, amesema kuwa mafunzo haya yataboresha utendaji kazi kwa kuwa yanaendeshwa na wakufunzi kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na makosa ya kifedha.
SSP Laizer ameongeza kuwa mafunzo haya ni mwendelezo wa program ya mafunzo kwa wapelelezi yanayoendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha makosa ya kifedha yanadhibitiwa ipasavyo na wahalifu wanachukuliwa hatua stahiki.



