Wananchi wanufaika vituo vya uwezeshaji

DODOMA: VITUO vya Uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini vimeendelea kuwa kimbilio la wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima na vijana wanaotaka kuanza biashara wenye mlengo wa kupiga hatua katika shughuli zao za uzalishajimali.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC), Gwakisa Bapala amesema hayo wakati akielezea mafanikio endelevu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Bapala amesema vituo hivyo vinaratibiwa na kusimamiwa NEEC, vimekuwa vikitoa huduma za mikopo rafiki, dhamana za mikopo, urasimishaji wa biashara, mafunzo ya ujasiriamali, usajili wa vikundi, taarifa za zabuni na masoko na huduma za teknolojia ya viwanda.
Amesema hadi kufikia Desemba 2025, Vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi vilikuwa 29 ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo vilikuwa 27.
Amesema Vituo hivyo vipo katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Kigoma, Dar es salaam, Tabora,Tanga, Singida,Pwani, Morogoro,Katavi na Rukwa na kwamba jitihada zikiendelea kufanyika ili vituo hivyo viweze kusambaa nchi nzima.

Bapala amesema katika kipindi cha kutoka mwezi Januari mpaka Desemba 2025 waliweza kuwafikia wanufaika 49,828, wanawake wakiwa 24,712 na wanaume 25,166 katika nyanja za mikopo, ya mafunzo ya ujasiriamali, urasimishaji wa biashara, ushauri wa kitaalamu na usajili wa vikundi vya kifedha.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo amesema jumla ya Sh Bilioni 15.1 zilitolewa kupitia vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa wajasiriamali 1,435.

Kati yao wanawake walikuwa 731 na wanaume 704 ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo mikopo iliyotolewa ilikuwa sh Bilioni 7.09 kwa wajasiriamali 341 ambapo wanawake walikuwa 164 na wanaume 177.
“Ongezeko la viwango vya mikopo na idadi ya wanufaika imetokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya sita ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kupanua huduma za Mifuko ya Uwezeshaji kushuka chini “amesema.
“Mikopo imewafikia wananchi wengi zaidi kupitia Vituo vya Uwezeshaji ambavyo vimeanzia katika ngazi za Halmashauri” amesema Bapala.
Mbali na hilo amesema jumla ya biashara 23,928 ziliweza kurasimishwa na Mamlaka rasmi za Serikali na lengo ni kusaidia wajasiriamali kuondoka kwenye masoko holela na kuingia kwenye ushindani wa masoko ya Kimataifa.
“Vituo vyetu vimekuwa vikifanya kazi hii ya urasimishaji wa biashara maana ni moja kati ya njia inayoweza kusaidia biashara zetu kuaminika na kupata masoko makubwa ya Kimataifa”amesema Bapala.
“Tunafahamu kuna vikwazo vingi wanakutana navyo wajasiriamali na ndiyo maana mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa vituoni huambatana moja kwa moja na zoezi la urasimishaji wa biashara zao”amebainisha Bapala.
Anatumiq nafasi hii pia kuwaomba vijana wachukue hatua ya kuvitembelea vituo vya uwezeshaji ili kujifunza na kuona fursa mbalimbali ambazo zinaweza kusawadia kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Bapala amesema Taasisi zilizomo ndani ya Vituo vya Uwezeshaji Kiuchumi ni SIDO, TRA, VETA, Mfuko wa Self , Mfuko wa Kilimo wa Pass Trust, Mfuko wa Pembejeo wa AGTF, OSHA,TBS ,Benki ya NMB,Chuo Kikuu Huria (OUT), TCCIA, TWCC, GS1Tanzania , Taasisi za RUDIDEO na B2B.



