“Ukiingia na gari baa uwe na kitambulisho maalumu”

NJOMBE: KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mahamoud Hassan Banga, amewataka wamiliki wa kumbi za starehe, masoko na baa kuhakikisha kuwa kila mtu anayeingia na chombo cha moto anakuwa na kitambulisho maalumu. Hatua hii inalenga kupunguza matukio ya wizi wa vyombo vya moto, hasa nyakati za usiku.
Agizo hilo limetolewa leo Machi 12, 2025, katika kikao kazi na maofisa usafirishaji wa mkoa huo, ambapo Kamanda Banga pia amewataka maofisa usafirishaji kufunga mifumo ya Tehama kwenye vyombo vyao vya moto ili kurahisisha upatikanaji wa vyombo hivyo endapo vitaibiwa au kuporwa na wahalifu.
Aidha, amewasihi maofisa hao kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani, hasa wakati wa usiku, na kufuata sheria za usalama barabarani bila kushurutishwa.
Pia, amewakumbusha kuepuka kushawishi au kutoa rushwa kwa maafisa wa usalama wa barabarani, huku akisisitiza kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria na hakivumiliki.
Sambamba na hayo, Kamanda Banga amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi mkoani Njombe limejipanga kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu, hivyo ametoa wito kwa maofisa usafirishaji kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi ili kuchagua viongozi waadilifu na wenye uwezo wa kuongoza jamii kwa haki.
Mwisho, Kamanda Banga amewataka maofisa usafirishaji kuwa waangalifu wanapopita katika eneo la Mjimwema kwa kuwa limekuwa na matukio mengi ya ajali, hususan zinazohusisha pikipiki, na kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara zaidi.



