Mkemia aongeza ufanisi bandarini

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imechangia ufanisi wa bandari za Dar es Salaam na Tanga kwa kuongeza shehena za mizigo inayoingia nchini na kwenda nchi jirani, zikiwamo za kemikali zinazotumika migodi ya madini.

Hayo yamebainishwa Dodoma na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko kwenye mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Dk Mafumiko alisema shughuli za uchimbaji madini ndani na katika nchi jirani zimechangia kuwezesha biashara ya kemikali zinazotumika kwenye uchimbaji huo kuongezeka, lakini pia, bandari za nchini kuneemeka kwa kusafirisha kiwango kikubwa cha kemikali hizo, hivyo kuongeza sehena ya mizigo inayohudumiwa.

“Kuna biashara ya kemikali za kimkakati zinazotumika kwenye uchimbaji na uchenjuaji madini ndani ya nchi na nchi jirani, ambazo ni pamoja na Amoniam Nitrate ambayo shehena imeongezeka katika Bandari ya Tanga kutoka tani 135,445 mwaka 2021/22 hadi kufika tani 359,629 mwaka 2024,” alisema Dk Mafumiko.

Alisema uingizaji wa kemikali hiyo katika Bandari ya Tanga umeongeza thamani ya bandari hiyo sambamba na kuongeza ufanisi wake.

Aidha, alitaja kemikali nyingine inayoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam ni salfa inayotumika kwenye uchenjuaji wa shaba katika nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo imeongezeka kutoka tani 396,982 mwaka 2021/2022 hadi tani milioni 1.36 mwaka jana.

Kemikali nyingine ni sianidi ya sodiamu (sodium cyanide) inayotumika kuchenjua madini Zambia na hapa nchini nayo imeongeza shehena katika Bandari ya Dar es Salaam na uingizwaji wake kupitia bandari hiyo ulikuwa tani 41,461 mwaka 2021/2022 hadi kufika tani 53,059 mwaka jana.

“Ongezeko la kemikali hizi zinazoingia kupitia bandari zetu na sisi kuzisimamia kwa kutoa vibali na kukagua, zimeongeza ufanisi wa bandari zetu hivyo kuleta tija,” alisema Dk Mafumiko.

Aidha, eneo jingine la mafanikio katika mamlaka hiyo ni uimarishaji na uchunguzi wa sampuli za kimaabara na kuwa
wameongeza sampuli kutoka 155,117 mwaka 2021/2022 hadi sampuli 188,392 mwaka jana.

Alisema ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya uchunguzi, ubora wa huduma, ushirikiano baina ya taasisi nchini likiwemo Jeshi la Polisi na wadau wengine wa afya.

“Uelewa wa wananchi na uwepo wa mashine na mitambo ya kisasa ya kufanya uchunguzi wa sampuli, umechangia kuboresha utoaji huduma za mashauri ya jina, utatuzi wa migogoro ya familia, utambuzi wa miili ya wahanga iliyoharibika katika majanga ya kitaifa,’’ alisema Dk Mafumiko.

Alisema katika hilo, mifano halisi ya karibuni ni majanga yaliyotokea Kariakoo, Dar es Salaam kwenye jengo lililoporomoka, walichukua sampuli za miili na kurahisisha utambuzi, na tukio la Mbinga mkoani Ruvuma ambako ajali ya gari iliyowaka moto na kuteketeza watu wote waliokuwemo.

Aidha, alisema mafanikio mengine waliyopata ni kwenye eneo la utambuzi wa jinsi tawala kwa watoto waliozaliwa na jinsi zenye utata.

Akizungumzia uwekezaji kwenye mitambo na uchunguzi, Dk Mafumiko alisema serikali katika kipindi hicho
imewezesha ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa, hivyo kuboresha huduma watoazo.

Alisema GCLA imenunua mitambo mikubwa 16 na midogo 274 yenye thamani ya Sh bilioni 18.4 na hivyo kurahisisha shughuli za uchunguzi na ufanisi, lakini pia mamlaka hiyo imechangia kutoa ushahidi wa kitaalamu wa mashauri 6,989 mahakamani, hivyo kuchangia utoaji wa haki kwa wakati.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button