Wasira atoa neno wapinzani kuzuiliwa kuingia Angola

KUTOKANA na hatua ya kuzuiwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani wa Tanzania kuingia nchini Angola, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewataka viongozi hao wasiinyooshee kidole serikali.
Wasira ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuzuiliwa na mamlaka za Angola kuingia nchini humo Machi 13.
Wasira alieleza hayo alipozungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika ukumbi wa Kanisani, Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe ambako anaendelea na ziara ya kikazi.
“Leo nimesoma viongozi walikuwa wanaenda Angola lakini wamenyang’anywa pasipoti huko ni Angola si hapa, hapa hatujawanyang’anya pasipoti na hata ikimaliza muda wake tunawapa ili waende wanakotaka halafu warudi salama.
“Wamelalamika kwa nini serikali imekaa kimya, kwani sisi tunasimamia Airport (Uwanja wa Ndege) ya Angola? Ariport ya Angola inasimamiwa na watu wa Angola, na pia huenda walikuwa na jambo lao ambalo lilitiliwa shaka. Wangeuawa tungesema kwa nini wamewaonea watu wasiokuwa na hatia,” alisema.
Aliongeza: “Sasa kuwaambia tu msiingie kuna tatizo gani si mrudi tu nyumbani”.
Mbali na Othman na Lissu, viongozi wengine waliozuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de
Fevereiro jijini Luanda ni marais wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu mstaafu wa Lesotho na
baadhi ya wakuu wa vyama vya siasa kutoka baadhi ya nchi za Afrika.
Viongozi hao, walikwenda Angola kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD) yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation yakiwa na lengo la kuwakutanisha wadau kutoka Afrika kwa madai ya kujadili demokrasia na kubadilishana uzoefu.



