Mwanafunzi auawa kikatili Rombo

KILIMANJARO: JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Kijiji cha Kirwa, Wilaya ya Rombo, kwa tuhuma za kumuua mtoto Rosemary Mathias (6) kwa kumtenganisha kichwa na kiwiliwili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeeleza kuwa, Rosemary, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mahaheni na mkazi wa Kijiji cha Mrere, alishambuliwa na mtuhumiwa Machi 15, 2025, majira ya saa tisa alasiri.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimkuta binti huyo akicheza na watoto wenzake kisha akamkata shingoni kwa kitu chenye ncha kali, na kusababisha kichwa chake kutenganishwa na kiwiliwili.
Kwa mujibu wa mashuhuda, siku ya tukio hilo, mtuhumiwa alirejea nyumbani kwao baada ya matembezi akiwa ameshika panga. Alianza kuwatafuta watoto waliokuwa wakicheza na hatimaye alimkamata Rosemary na kutekeleza mauaji hayo.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea, na mara utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.



