Watakiwa kutumia vifaa vya kisasa vya uokoaji

WAMILIKI na waendeshaji wa maboti yanayofanya shughuli zake katika Ziwa Tanganyika wametakiwa kutumia vifaa vya kisasa vya uokoaji majini ikiwemo maboya na makoti ya kujiokolea ‘Life jacket’ badala ya kutumia madogoro na madumu.

Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) makao makuu, Adam Mamilo amesema hayo mkoani Kigoma katika mkutano wa pamoja na wamiliki wa maboti, mabaharia na wadau wa usafirishaji majini ziwa Tanganyika kukumbusha kufuata taratibu za usalama za uendeshaji wa vyombo vya majini ili kuzuia ajali.

Mamilo amesema kuwa pamoja na kazi kubwa ya ukaguzi na usimamizi wanaofanya lakini bado wapo wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya majini wanaokiuka sheria hizo hivyo TASAC imekuwa ikichukua hatua kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kuitisha mikutano ya pamoja kama huo kukumbusha kila upande kutimiza wajibu wake.

Akizungumza suala la kituo cha uokoaji amesema kuwa kwa sasa hakuna kituo cha uokoaji mkoani Kigoma na kwamba shirika hilo lina mpango wa kujenga kituo cha uokoaji katika ziwa Tanganyika kama ilivyo kwenye maziwa mengine nchini ili kusaidia ajali inapotokea na kwamba mchakato wa mradi huo umeshaanza ambao utaenda sambamba na uimarishaji wa minara ya mawasiliano kwenye mwambao wa ziwa.

Mmoja wa wamiliki aliyehudhuria mkutano huo, Mussa Issa amesema kuwa wamekuwa wakipata hasara inapotokea dhoruba ziwani kwa kushindwa kupata mawasiliano ya watu waliopo kwenye boti ziwani ambapo kama mawasiliano yangepatikana ingeweza kuwa rahisi kuwaokoa.

Naye Kashindi Adamu amesema kuwa ni lazima serikali iliangalie suala hilo kwa makini kwani kwa sasa hakuna kituo cha uokoaji Ziwa Tanganyika hivyo kuwepo kwa mawasiliano ya simu inaweza kusaidia kukabili tatizo linapotokea na kuomba serikali kuimarisha minara ya mawasiliano eneo kubwa la mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button