Unywaji maziwa, ulaji mayai vijijini Changamoto – tafiti

WATAFITI kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameeleza ya kwamba wananchi wengi wanaoishi vijijini katika Wilaya ya Kilombero na Mvomero mkoani Morogoro hawali mayai wala kunywa maziwa licha ya kufuga kuku, ng’ombe na mbuzi.

Mkuu wa Mradi wa Kilimo, Chakula na Lishe (FoodLAND), Profesa Suzan Nchimbi kutoka SUA amesema hayo kwa niaba ya watafiti wenzake wakati akizungumza na Waandishi wa Habari alipokuwa akitoa matokeo ya utafiti wa mradi huo uliotekelewa kwa muda wa miaka minne na nusu hadi kufikia 2025.

Profesa Nchimbi amesema hali hiyo inawafanya wananchi hao kuwa kwenye uhatarishi mkubwa wa kukosa virutubishi muhimu vinavyosaidia kuujenga mwili kiafya.

“ Mradi huu ulilenga utafiti wa chakula na lishe , watu wanazalisha chakula ili kiweze kuliwa , lakini tumeona kwa muda mrefu katika nchi yetu pamoja na kwamba tunajitoshereza kwa chakula lakini kunamatatizo ya ulaji wa chakula” amesema Profesa Nchimbi .

Profesa Nchimbi amsema kwa sasa hivi kuna matatizo ya kupata vyakula vya aina mbalimbali na watu kula vyakula vya aina mbalimbali mchanganyiko.

Alisema katika kitumiza lengo kuu la mradi walifanya tafiti mbalimbali kuhusu kilimo na chakula na baadhi yake zimeanishiwa kwenye matokeo ya utafiti huo baada ya kufanyika kwenye mkoa wa Morogoro katika wilaya ya Kilombero na Mvomero.

Profesa Nchimbi amesema utafiti uliofanyika Wilaya ya Kilombero na Mvomero na kwa Mvomero ni katika kijiji cha Ndole, kata ya Kinda na ulifanywa kwa njia mbalimbali ikiwemo ya madodoso.

Katika matokeo ya utafiti huo ulibaini kuwa wananchi wa vijijini wamekuwa wakifuga kuku wa mayai kwa dhumini la kibiashara zaidi ambapo mayai wamekuwa wakiuza ili kujipatia fedha kwa ajili ya kutumia kwenye matumizi mengine.

“ Matokeo ya utafiti umegundua hasa vijijini ulaji wa vyakula vyenye asili yanprotini yakiwemo mayai ni mdogo pamoja na maziwa, kati ya watu waliowahoji kama 500 ilionekana sio wengi wanakula mayai na sio watu wengi wanakunywa maziwa , karibu ya asilimia zaidi ya 60 ya waliohojiwa ulaji wao mayai na unywaji wa maziwa ni mdogo “ anasema

Mratibu wa mradi huo pia anasema utafiti wao ulibaini kwenye unywaji wa maziwa wananchi wengi hasa wa vijijini hawanywi maziwa kwa sababu hawafugi ng’ombe na mbuzi wa maziwa.

Profesa Nchimbi amesema walifanya utafiti uliohusu tabia za walaji wa vijijini hususani lishe ya mama na mtoto katika wilaya ya Mvomero, mjini wa Morogoro na Dar es Salaam kwa kukusanya takwimu za taarifa mbalimbali kwa wananchi.

“ Tulifanya utafiti kwa walaji wa vijijini na wa mijini hasa kuhusiana na lishe ya mama na mtoto na tukapata matokeo ya tabia za walaji na matokeo yake yametumika kutengeneza mapendekezo ya namna gani watu wale chakula” anasema Profesa Nchimbi.

Profesa Nchimbi amesema kwa matokeo ya awali waliweza kuona kwamba watu wa mjini na vijijini ulaji wao wa chakula uko tofauti kidogo na vitu vingine vilivyogundulika kwamba zamani watu walifikiri vijijini hawali vitu vya mafuta kwa wingi na pia hawali sukari kwa wingi.

“ Kupitia utafiti huu tumegundua hata vijijini sasa hivi watu wanakula vyakulaa vya kukaanga kwa wingi na hivi vyakula vya kukaaga na mafuta mengi vinasababisha matatizo mbalimbali za kiafya “ anasema Profesa Nchimbi.

Profesa Nchimbi anasema kupitia utafiti huo wametoa mapendekezo kuhusu namna bora ya kuboresha ulaji wa chakula kwa ajili ya afya bora ili kutekeleza kampeni ya kitaifa ya kutoa mwamko kwa walaji kuhusu ulaji bora wa chakula kwa afya bora.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button