Bil 7.3/- zahitajika kufufua kiwanda cha ushirika Geita

CHAMA Cha Ushirika Mkoa wa Geita (GCU) kimeweka wazi kuwa zinahitajika jumla ya Sh bilioni 7.3 kwa ajili ya kufufua kiwanda cha kuchakata pamba kilichopo kata ya Kasamwa wilayani Geita mkoani hapa.
Mwenyekiti wa GCU aliyemaliza muda wake, Zainabu Mahenge amesema hayo jana akiwa Kasamwa mjini Geita katika mkutano mkuu wa chama hicho uliokuwa na ajenda kuu ya kufanya uchaguzi na kupata uongozi mpya.
Amesema kati ya gharama hizo kiasi cha Sh bilioni 1.3 ni kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa mashine za kiwanda huku kiasi cha sh bilioni sita ni bajeti ya ununuzi wa pamba pamoja na uendeshaji wa kiwanda.
Amesema ufufuaji unatarajiwa kuanza Aprili 2025, lakini wameshafikia makubaliano ya awali na benki ya AZANIA ambayo imeonyesha nia ya kuwasaidia na kinachosubiriwa ni kibali kutoka ofisi ya MRAJIS.

“Kwa sababu wenye mali ni wanachama, kwa hiyo muhtasari ukiridhia huo muhtasari tutakuwa nao, utaainisha ukomo wa madeni, tutapeleka kwa MRAJIS utaidhinishwa ili tupeleke benki”, amesema.
Kaimu Mrajis Msaidizi mkoa wa Geita, Menance Chandika amesema mpaka sasa viwanda vya ushirika Chato na Bukombe ndio vinafanya kazi lakini bado kuna changamoto ya uhaba wa malighafi.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Dk Alfred Msenya amesema serikali inafanya juhudi tofauti kuimarisha uhai wa vyama vya ushirika kwa kurejesha na kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Amesema tayari mfumo wa stakabadhi ghalani umeanza kutumika kwenye mazao ya dengu na choroko na utaenda kwenye mazao mengine ili kutengeneza bei rafiki ya mazao na kuchagiza kilimo chenye tija.
Amesema kwa kupitia mfumo huo zabuni ya mazao itatangazwa kidijitali ili kupokea ushindani wa wanunuzi ambapo itamsaidia mkulima kunufaika na serikali kupata tozo ya mauzo ya maduhuli.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Geita, ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dk Omari Sukari amepongeza GCU kwa kupata hati safi na kuwataka viongozi kusimamia maono ili kufikia adhima ya kufufua viwanda vya pamba.



