MNH yapokea vifaa tiba kutoka Al Muntazir Sekondari

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea msaada wa vifaa tiba na kufundishia kutoka Al Muntazir Islamic International School,ikiwa ni kuboresha huduma kwa watu wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za afya ya akili katika hospitali hiyo.

Akizungumza leo Aprili 23,2025 wakati wa kukabidhi msaada huo mshauri wa shule (school counsellor), Sayyida Tehsin amesema kwa kutambua umuhimu wa afya ya akili hasa kwa watoto na vijana, shule hiyo iliona ni vyema kutoa mchango huo ili kusaidia kuwapa faraja na matumaini wagonjwa wa afya ya akili waliopo MNH.

Aidha, wanafunzi wa shule hiyo walioshiriki katika kukabidhi msaada huo walipewa elimu ya afya ya akili na wataalamu kutoka MNH, ikiwa imelenga kuwajengea uelewa juu ya umuhimu wa afya ya akili, namna ya kutambua viashiria vya matatizo ya kiakili, na jinsi ya kusaidia wenzao wanaokumbwa na changamoto hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Afya ya Akili kutoka MNH, Dk Praxeda Swai ameshukuru uongozi wa shule hiyo pamoja na wanafunzi kwa kujitoa kwao kusaidia jamii, akisisitiza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya matibabu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.




