THRDC: Polisi boresheni utaratibu wananchi kuingia mahakamani

DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umetoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama kwa ujumla kuweka utaratibu mzuri kwa wananchi kuhudhuria mashauri mahakamani, huku wakisisitiza kuwa ni haki ya kikatiba kwa kila mtu kushiriki au kufuatilia mwenendo wa kesi mahakamani.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, jijini Dar es Salaam kufuatia vurugu zilizotokea siku ya jana nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Vurugu hizo zilitokana na zuio la polisi kwa baadhi ya watu, wakiwemo viongozi, kushindwa kuingia mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambapo pia taarifa zisizo rasmi zinasema baadhi ya watu walijeruhiwa.

Wakili Olengurumwa amesema ni haki ya kila mtu kufika mahakamani kusikiliza kesi, hasa inapomhusu kiongozi wa kitaifa kama Tundu Lissu, kwani wananchi wana haki ya kujua hatma ya mashitaka dhidi ya viongozi wao.

SOMA ZAIDI: THRDC yataka mazingira bora kuelekea Uchaguzi Mkuu

Aidha, Olengurumwa amesisitiza haja ya kufanyika kwa mkutano wa kitaifa wa maridhiano utakaowakutanisha makundi yote muhimu nchini, wakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa, serikali, vyombo vya dola, msajili wa vyama vya siasa na taasisi nyingine ili kufikia mwafaka wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Katika wito wake kwa pande zote, Olengurumwa amevitaka vyama vya upinzani, hususan CHADEMA, kuwa tayari kushiriki mazungumzo, huku akiwasihi viongozi wa CCM kutambua umuhimu wa majadiliano kwa ajili ya ustawi wa taifa.

Pia, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutumia kwa vitendo mfumo wake wa 4R na mamlaka aliyonayo kuondoa mvutano wa kisiasa unaoendelea nchini.

Ikumbukwe kuwa, siku moja kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilitoa tamko la kupiga marufuku mikusanyiko isiyo halali baada ya kupata taarifa kuwa wafuasi wa CHADEMA kuwa walipanga kukutana kwa lengo la kushinikiza kuachiwa huru kwa mwenyekiti wao, Tundu Lissu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button