DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetoa mapendekezo matatu muhimu kuhusu umuhimu wa kuafikiwa kwa muafaka wa kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuweka mazingira bora ya uchaguzi huru na wa haki.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema muafaka huo utasaidia kuondoa hofu na sintofahamu zinazojitokeza katika kipindi cha uchaguzi.
Aidha, amependekeza kuhusishwa kwa makundi yote ya kijamii ikiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa na taasisi za kiserikali kwa ajili ya majadiliano ya pamoja yatakayosaidia kushughulikia changamoto zilizopo kabla ya uchaguzi. Majadiliano hayo yanapaswa kusimamiwa na wazee wenye uzalendo na busara.
Wakili Olengurumwa amepongeza jitihada na maboresho yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, hususan katika maeneo ya uchaguzi, kama vile kubadilika kwa mfumo wa baadhi ya wagombea kupita bila kupingwa, jambo ambalo lilikuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu.
Mojawapo ya mapendekezo muhimu yaliyotolewa na THRDC ni kuanza mapema kwa mchakato wa muafaka wa kitaifa, ili kutoa nafasi kwa vyama vya siasa na wananchi kujiandaa kikamilifu na uchaguzi badala ya kutumia muda mwingi kudai maboresho ya mfumo wa uchaguzi.
Aidha, THRDC imesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa hoja za msingi ndani ya mchakato wa muafaka huo, ikizingatiwa kuwa kumekuwa na matatizo yanayojirudia kila uchaguzi, na kuathiri kwa kiasi kikubwa uhalali wa mchakato mzima wa uchaguzi.
SOMA ZAIDI: Mtandao wa Wanawake watoa msukumo kwa nafasi za uongozi
Wakili Olengurumwa ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na: Kukimbia kwa wagombea wakati wa kurudisha fomu, Kusumbuliwa kwa mawakala wa vyama, Kuenguliwa kwa wagombea bila sababu za msingi pamoja matumizi ya vyombo vya dola kudhoofisha vyama vya upinzani.
Kwa mujibu wake, matatizo haya yanachangiwa na aina ya wasimamizi wa uchaguzi pamoja na matendo na mitazamo ya baadhi ya viongozi wa kisiasa wakati wa uchaguzi.
Katika hatua nyingine, THRDC imeainisha masuala 10 muhimu yanayopaswa kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025, ikiwa ni pamoja na: wasimamizi wa uchaguzi wasiwe watumishi wa serikali pekee, tabia za maafisa wa uchaguzi kufunga ofisi hasa wagombea wa uchaguzi wanaporudisha fomu wakati wa uchaguzi, wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa, makosa ya kiuchaguzi kutambulika kama makosa ya jinai, mapungufu ya sheria na kanuni za uchaguzi pamoja na suala la usalama wa kura na utoaji wa matokeo.
Kwa kumalizia, THRDC imewasihi wadau wote wa uchaguzi wakiwemo viongozi wa kisiasa, dini, wagombea, wananchi na wasimamizi wa uchaguzi kuona umuhimu wa kuafikiana kitaifa. Lengo ni kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2025 unafanyika katika mazingira ya utulivu, uhuru na haki kwa pande zote.