Mtandao wa Wanawake watoa msukumo kwa nafasi za uongozi

MRATIBU wa Kitaifa wa Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu (CWHRDS), Hilda Dadu amesema mtandao wake unaendelea kutoa elimu kwa wanawake ili kuongeza nafasi zaidi sehemu za uongozi, kumiliki mali na kujifungua kwenye mazingira salama.

Alisema hayo jana jijini hapa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu.

Alisema wanawake wamekuwa na uthubutu kutoka ili kwenda mbele linapokuja suala la kudai haki.

“Kwa hivi karibuni, tumechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa wanawake sehemu za uongozi, kumiliki mali na hata kujifungua kwenye mazingira salama,” alisema.

Alisema mpaka sasa wameweza kuwafikia wanawake watetezi 120 ambao wamejengewa uwezo kuhusu haki za binadamu.

“Tumetoa misaada ya kisheria na misaada ya kibinadamu kwa wale waliokutana na madhila hasa wakati wa kutetea haki za wanawake na makundi maalumu,” alisema.

Alisema wanawake watetezi walikuwa mstari wa mbele lakini mazingira ya kufanyia kazi bado yana changamoto kubwa.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Anne Malipula alisema wanawake watetezi wa haki za binadamu wana nafasi kubwa katika kukuza na kulinda haki za binadamu.

“Serikali inatambua mchango wenu wa kuboresha maisha ya wanawake wa Tanzania, mnaisaidia sana serikali kufuatilia haki za wanawake na wasichana,” alisema.

Mwakilishi kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Lissa Kagaruki alisema kuwa wanawake watetezi wanapitia changamoto nyingi.

“Kabla ya mwaka 2019 watetezi wanawake walikuwa waoga sana lakini kupitia mitandao wamekuwa na ujasiri,” alisema.

Pia alisema hakuna sheria inayotambua utetezi wa haki za binadamu.

“Tunahitaji sheria inayosimamia, inayomtaja mtetezi wa haki za binadamu ni nani,” alisema.

Mkurugenzi kutoka Idara ya sheria wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nagu Assey alisema kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha watetezi hawanyanyaswi na hawatishwi.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x