Serikali yaondoa zuio mazao kutoka Malawi, Afrika Kusini
SERIKALI imetangaza kuondoa zuio la biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo kati ya Tanzania na nchi ya Malawi na Afrika Kusini, kuanzia jana.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe baada ya mazungumzo ya kidiplomasia yaliyofanyika kati ya pande zote tatu kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Aprili 17, 2025 Serikali ya Malawi ilitoa tamko la kuzuia uingizwaji wa baadhi ya mazao kutoka Tanzania, yakiwamo mahindi, mchele, ndizi na tangawizi.
Kutokana na hatua hiyo, Serikali ya Tanzania ilitoa onyo kwa nchi hizo mbili kuwa endapo hazitarekebisha uamuzi huo ndani ya siku saba, Tanzania ingezuia uingizaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini.
Hata hivyo, baada ya nchi hizo kushindwa kuondoa vizuizi, Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo, Aprili 23, 2025 ilitangaza rasmi marufuku ya kuingiza mazao ya kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini na kusitisha usafirishaji wa bidhaa hizo kupitia Tanzania kuelekea nchini Malawi.
Zuio hilo lilihusisha pia, usafirishaji wa mbolea iliyokuwa itumike katika msimu ujao wa kilimo nchini Malawi.
Bashe alisema kutokana na mawasiliano rasmi kutoka kwa nchi hizo mbili na nia yao ya kushiriki majadiliano ya pamoja, Serikali ya Tanzania imeamua kuondoa vizuizi vyote ili kutoa nafasi kwa mchakato wa kidiplomasia kuendelea.
“Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Aprili 26, 2025 (jana) tukiamini kuwa majadiliano yanayoendelea yatatoa suluhisho la kudumu,” alisema Bashe.
Alifafanua kuwa Serikali ya Malawi imethibitisha kutuma ujumbe rasmi utakaowakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo, kwa ajili ya kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma Mei 2, 2025.
Kuhusu Afrika Kusini, Bashe alisema majadiliano kati ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu na mamlaka husika za Afrika Kusini, yanaendelea kwa lengo la kuhakikisha masuala ya afya ya mimea na masoko yanatatuliwa kwa masilahi ya pande zote.
Bashe aliwahakikishia Watanzania, hususani wakulima, kuwa serikali itaendelea kulinda masilahi ya taifa, kuhakikisha biashara huru na yenye tija kwa mazao ya kilimo inafanyika kwa kuzingatia kanuni za afya ya mimea, rasilimali za nchi na uhusiano wa kidiplomasia.


