JK ashiriki mafunzo ya mawaziri Harvard

BOSTON : RAIS Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete yuko Boston nchini Marekani, akishiriki katika mafunzo ya Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Mipango kutoka nchi zinazoendelea.
Mafunzo hayo yanafanyika chini ya Mpango wa Uongozi wa Ngazi ya Mawaziri wa Chuo Kikuu cha Harvard, maarufu kama Harvard Ministerial Leadership Program.
Dk. Kikwete ni miongoni mwa viongozi wastaafu wa kitaifa walioteuliwa kama wakufunzi ambapo watatumia uzoefu wao kuwajengea uwezo viongozi wa kizazi kipya.
Mafunzo haya yanashirikisha pia Wakuu wa Taasisi za Kimataifa, wawakilishi wa mashirika binafsi na mabingwa wa sera, uchumi na maendeleo kutoka duniani kote.



