Bonanza la Mac D Fun Run 2025 laiva

DAR ES SALAAM: BONANZA LA Mac D Fun Run 2025 msimu wa pili linatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi, Juni 7, katika viwanja vya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Kunduchi, Dar es Salaam.
Tukio hili maalum litajumuisha mbio za kujifurahisha (Fun Run) pamoja na mchezo wa mpira wa miguu utakaokutanisha timu ya Mac D na IPP Media.
Kwa mujibu wa Mratibu wa bonanza hilo, Deogratius Rweyunga, shughuli zitazinduliwa mapema saa 12:00 alfajiri kwa mbio za pole ambazo zitahusisha wadau mbalimbali.

Rweyunga amesema lengo kuu la mbio hizo ni kuhamasisha afya njema na ushiriki wa jamii bila kuzingatia ushindani.
“Hakutakuwa na mshindi wala zawadi, bali washiriki wote watapewa fulana (T-shirt) za bure kwa ajili ya kushiriki mbio hizi,” amesema.
Baada ya mbio kumalizika, saa 10:00 jioni kutafanyika pambano kali la mpira wa miguu kati ya timu ya Mac D na kikosi cha IPP Media. Mshindi wa mechi hiyo atapewa kombe kama ishara ya ushindi na ushiriki bora.



