Madiwani wampongeza Samia utekelezaji miradi Kigoma

KIGOMA: BARAZA la Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu limemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri ya kuleta fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Kutokana na hilo, baraza hilo limeamua kuchangia Sh milioni 1 kwa ajili ya Rais Samia kuchukua fomu ya kugombea urais. Aidha Sh 577,000 imechangwa kwa ajili ya Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Vuma Olle kuchukua fomu ya kugombea ubunge.

Akizungumza katika kikao cha robo ya tatu cha baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Eliya Kagoma amesema ni ukweli usiopingika kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ya maendeleo wilayani humo.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dk Semistatus Mashimba akizungumza kwa niaba ya watendaji wa halmashauri amesema wanaungana na baraza hilo kumpongeza Rais.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kasulu, Jennifer Chinguile amepokea mchango huo kwa niaba ya chama na kuahidi kuuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Emmanuel Nchimbi kabla ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika badaaye mwezi huu.

Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Simon Nzibuje ametoa shukrani kwa mchango huo na kuhaidi kuufikisha kwa mhusika.

Akitoa salamu za serikali, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Mwakisu amewataka wananchi kuwa na tahadhari na kuhakikisha wanatunza chakula kutokana na hali isiyoridhisha ya usalama wa chakula kwa sasa.



