Chino Kid kufanya kolabo ya kimataifa

DAR ES SALAAM : STAA wa muziki wa Bongo Fleva, Chino Kid, anatarajia kutoa kolabo mpya na msanii anayeishi Marekani, Mudara, ikiwa ni jitihada za kukuza wigo wa muziki huo katika ukanda wa Afrika Mashariki na diaspora.
Akizungumza na HabariLEO, Mudara amesema kolabo hiyo tayari imekamilika na inatarajiwa kutoka muda wowote kuanzia sasa, akibainisha kuwa itakuwa chachu ya mafanikio zaidi katika sanaa yake ya muziki.
“Inajulikana Chino hana kazi mbovu na mimi pia nimeonyesha uwezo wangu mwingine kwenye hii ngoma. Ikitoka, naamini itanifungulia milango mipya na kuniongezea mashabiki kwenye kanda ya Afrika Mashariki,” amesema Mudara.
Mudara, ambaye kwa sasa anafanya kazi zake za muziki nchini Marekani, amesema wimbo wake unaojulikana kama Osiyaa umemfungulia fursa nyingi za kusikika katika vyombo vikubwa vya habari hapa nyumbani, jambo lililompa msukumo wa kuwekeza zaidi katika kolabo na wasanii wa Tanzania.
“Nimeamua kutumia gharama kubwa kuipata hii kolabo na Chino Kid kwa sababu naamini itanipa nafasi ya kupanua namba zangu kwenye majukwaa ya kidijitali kama YouTube, Boomplay na Audiomack,” amesema.
SOMA: Nyashinski kukiwasha kesho Dar
Aidha, amesema ataendelea kushirikiana na wasanii wa Tanzania licha ya kuishi nje ya nchi, akibainisha kuwa anathamini mapokezi makubwa anayoyapata kutoka kwa mashabiki wa Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, Mudara amepongeza mchango wa wasanii wakubwa wa Bongo Fleva kama Diamond Platnumz, Alikiba, Jux, Rayvanny, Harmonize, Abby Chams na wengine kwa kuendelea kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa.
Amesema sapoti wanayopata kutoka kwa serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa kichocheo kikubwa kwa wasanii kuendelea kufanya kazi bora na kupeleka sanaa hiyo mbali zaidi.