Wanafunzi Sekondari Mndimba Tandahimba wafundwa mapambano dhidi ya rushwa

MTWARA: KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mndimba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wakawe waadilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kiongozi huyo ametoa ushauri huo leo Mei 22, 2025 wakati Mwenge wa Uhuru ulipozindua bweni la wanafunzi la shule hiyo na klabu ya wapinga rushwa iliyopo shuleni hapo.
Amesema kuanzia sasa vijana hao wameshakuwa wazalendo, wakakamavu, viongozi na waadilifu juu ya kazi wanayoenda kuifanya huku akiwaomba walimu pamoja na wazazi kuwapatia ushirikiano wanafunzi hao kwani isiwe sababu ya kuwafelisha na kuwachukia wanafunzi hao juu ya kazi hiyo wanayoenda kuifanya.

“Tumekuja kujionea matumaini makubwa juu ya mabweni ya watoto wetu ambao watasoma kwenye shule hii ya sekondari ya mdimba, leo hii Mwenge wetu wa uhuru umekuja kuweka heshima juu ya mabweni yetu ambayo watoto wetu watasoma katika shule hii,” amesema Ussi.
SOMA ZAIDI: Mwenge wa Uhuru una historia ya kuvutia
Aidha, watoto hao licha ya kuja kupata elimu shuleni hapo lakini pia wanaendelea kujionea matunda ya kufundishwa mambo mbalimbali ambayo yataenda kuwasaidia siku za baadaye.
Hata hivyo kuhusu bweni hilo linalozinduliwa na mwenge huo litawasaidia vijana hao kupata elimu bora na sahihi kuhusu kile walichokipata kwenye shule hiyo.

Aidha, katika halmashauri hiyo
miradi mbalimbali sita ya maendeleo kupitiwa na Mwenge wa Uhuru yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 ikiwemo bweni hilo, mradi wa maji mivanga, Kituo cha Afya Kitama.
Pia mradi wa ujenzi wa barabara ya Masau-Athakwani na Mahakama ya Mkuruma, kuona na kukagua shughuli za bodaboda wa kikundi cha tuvene na mingine huku ukikimbizwa umbali wa kilomita 111.6 kwenye halmashauri hiyo.
Mkazi wa kijiji hicho, Maulidi Issa amesema serikali inaendelea kuwajali wananchi kwa kuwaletea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu ambapo sasa wanajionea Mwenge wa Uhuru unazindua mabweni kwa ajili ya kuwaondolea watoto wao changamoto ya kutembea kila siku kwenda shule.


