TPDC waendesha bonanza sekondari Mtwara

MTWARA: SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli (TPDC) limeendesha bonanza kwa wanafunzi kutoka baadhi ya shule za sekondari mkoani Mtwara kwa lengo la kuendeleza uhusiano na ujirani mwema katika shule hizo.
Akizungumza wakati wa bonanza hilo la wanafunzi mkoani humo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la TPDC, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Shirika hilo, Marie Msellem amesema TPDC inazidi kuendeleza uhusiano na ujirani mwema mashuleni ikiwa ni pamoja na kuanzisha klabu za TPDC zinazotoa elimu juu ya namna nzuri ya matumizi ya gesi asilia.
Aidha, bonanza hilo limefanyika katika Shule ya Sekondari ya Mangamba iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani ikijumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa pete, kukimbia kwenye gunia, kufukuza kuku.
Shule zilizoshiriki bonanza hilo ni Sekondari za Msimbati, Naliendele, Mangamba na Ziwani.
“TPDC inazidi kuendeleza uhusiano na ujirani mwema mashuleni ikiwa ni pamoja na kuanzisha klabu za TPDC zinazotoa elimu juu ya namna nzuri ya matumizi ya gesi asilia,”amesema Msellem.
Aidha,amewataka wanafunzi wa sekondari za Msimbati, Naliendele, Mangamba na Ziwani mkoani Mtwara kuwa mabalozi wazuri na walinzi wa miundombinu ya gesi asilia katika maeneo yanayowazunguka.
Bonanza hilo limetamatika kwa shule ya sekondari ya ziwani kwa kutwaa ubingwa katika mchezo wa mpira wa miguu kwa mikwaju minne ya penati dhidi ya wapinzani wake mangamba sekondari wakipoteza kwa penati tatu.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki bonanza hilo wameishukuru TPDC kwa kuandaa mashindano kwani kupitia michezo kama hiyo husaidia kuibua vipaji mbalimbali kwa vijana.
Wameongeza kuwa bonanza hilo limesaidia kuimarisha uhusiano mzuri baina ya shule moja na nyingine katika sekta ya micheza na taaluma hivyo wameiomba TPDC kuendeleza kuratibu michezo hiyo.



