Mwamba Mining wajitosa kuinua vipaji Geita

GEITA: KAMPUNI ya Mgodi wa Mwamba Mining iliyopo katika kata ya Nyarugusu wilayani Geita imezindua mpango maalumu wa kuinua na kuendeleza ujuzi, maarifa na talanta kwa watoto na vijana.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) ambapo dhamira kuu ni kuwawezesha watoto kufikia ndoto zao na vijana kuwajengea uwezo wa kujiajiri.
Ofisa Mahusiano wa Mgodi, Evance Rubara amebainisha hayo katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo uliofanyika katika uwanja wa Nyarugusu kwa kuanza na michezo ya mpira wa miguu na pete.

Evance amesema awamu ya kwanza ya mpango ni miaka mitano ikiwemo miaka miwili ya matazamio ambapo watajumuisha wahitimu wa shule na vyuo wenye talanta na ujuzi mbalimbali wasio na ajira.
Amesema kwa vijana ambao ni wahitimu wa vyuo lakini hawana cha kufanya watapatiwa nafasi ya kufanya kazi mgodini ili kujengewa uzoefu huku kwa wahitimu wa shule watajengewa uwezo na fursa ya kujiajiri.
“Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba nguvu mali tuliyonayo hapa, ambayo ni raslimali watu, nguvu ambayo inatoka kwa vijana, hii nguvu isiende kujenga sehemu nyingine, bali hii nguvu ibaki hapa”, amesema.
Meneja Mgodi wa Mwamba Mining, Calvin Habil amesema mpango huo ni mwendelezo wa kampuni kuhakikisha jamii inayozunguka maeneo ya mgodi inanufaika moja kwa moja na raslimali madini iliyopo.

Ameongeza kuwa, maono ya mgodi pia ni kutumia sekta ya madini kubadili maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla kwenye nyanja tofauti ikiwemo afya, elimu na michezo ambayo inazalisha ajira nyingi.
Calvin amesema mpango huo utashirikisha watalaamu kutoka nchi za Marekani, Uingereza na Afrika ya Kusini ili kufanikisha zoezi la utambuzi na uendelezaji wa vipaji hususani katika soka kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwamba Mining, Thomas Cornew amesema mpango huo unatarajiwa kujenga mahusiano bora baina yao na jamii ya mkoa wa Geita na kuchagiza uzalishaji wenye tija zaidi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyarugusu, Lusekelo Mwaikenda amekiri kuwa mpango wa Mwamba Mining utazalisha kizazi chenye tija na kupunguza changamoto ya uzururaji na wizi inayotokana na kukosa kazi.



