Wabunge wapendekeza itungwe sera moja ya kodi

DODOMA;WABUNGE wameshauri serikali kuandaa Sera ya Kodi moja ili kutoa mwongozo wa masuala yote ya kodi nchini.
Akisoma maoni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025, pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Twaha Mpembenwe, amesema kuna umuhimu wa kuwa na sera hiyo.
“Sera ni mkakati au mwongozo unaotumiwa na Serikali kupanga na kutekeleza ukusanyaji wa kodi. Sera inatoa maelekezo ya aina ya kodi na namna zitakavyokusanywa, viwango vya kodi pamoja na matumizi ya mapato yanayotokana na kodi.
“Pamoja na kwamba kuna sheria mbalimbali za kodi nchini, Tanzania haina sera ya kodi moja inayotoa muongozo wa masuala mbalimbali kama vile; utolewaji wa vivutio na misamaha ya kodi, utozaji, kuchochea ukuaji wa uchumi na ukuaji wa sekta mbalimbali pamoja na usimamizi wa kodi za ndani na za kimataifa.
“Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa sera hiyo kunasababisha nchi yetu kutokuwa na viwango vya kodi vinavyotabirika pamoja na kuongeza vitendo vya ukwepaji wa kodi.
“Hivyo, Kamati inaona kwamba kuna umuhimu wa kuandaa sera ya kodi ili kutoa mwongozo wa masuala yote ya kodi,” amesema Mpembenwe.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button