Kombe la Mapung’o kuinua vipaji vya soka Geita

MDAU wa maendeleo mkoani Geita, Paschal Mapung’o amejitosa kudhamini mashindano ya mchezo wa soka katika kata ya Nyakagwe wilayani Geita kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya vijana.
Mashindano hayo yanafahamika kama Mapung’o Cup yanafanyika kwa mara ya pili mfululizo tangu yalipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2024 kwa kushirikisha timu za ndani na nje ya mkoa wa Geita.
Uzinduzi wa mashindao ya Mapung’o Cup mwaka 2025 umefanyika katika uwanja wa Nyakagwe uliopo kata ya Nyakagwe kwa mchezo kati ya wenyeji Nyakagwe na Mabasi kutoka wilayani Kahama.
Mdhamini Mapung’o amesema matarajio yake ni kuona mashindano hayo yanatumika kama daraja la vijana wenye vipaji kuonyesha uwezo ili wapige hatua.
Amesema mashindano hayo ni matokeo ya vijana wenye maono na matamanio ya kujenga kizazi chenye ushindani katika soka na kutengeneza mazingira rafiki ya kufikia matokeo chanya.
“Tuna kijana mmoja kupitia mashindano haya ameweza kusajiliwa na timu kubwa nchini, yupo timu ya vijana, kwa hiyo timu nyingi wajitahidi kucheza vizuri, wawe na nidhamu watapata matokeo mazuri,”amesema.
Mratibu wa Mashindano, Marco Victor amesema kwa mwaka huu mashindano hayo yanashirikisha timu 17 kutoka maeneo ya mikoa ya Mwanza, Geita na Shinyanga.
Victor ametaja udhamini wa jumla wa mashindano hayo ni sh milioni 10 ambayo itahusisha zawadi kwa mshindi wa kwanza ambaye atapata sh milioni 5.3 na mshindi wa pili atapata sh milioni 3.5.
Ameongeza kuwa, kiasi kingine cha pesa kitagawanywa kwa vipngele vya zawadi ya mtu mmoja mmoja ambazo ni mchezaji bora, mfungaji bora, golikipa bora, kocha bora pamoja na mchezaji chipukizi.
Baadhi ya mashabiki kutoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga na wilaya ya Geita mkoani Geita wamekiri mashindano hayo kustashawisha vijana wengi kuacha uhalifu na kujikita katika michezo.



