Watanzania waalikwa mbio za Great Ruaha

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, amewataka wananchi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika mbio za Great Ruaha Marathon zitakazofanyika Julai 5, 2025, zikiwa na lengo la kukuza utalii wa Kusini na kutoa hamasa kwa jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Juni 17, 2025, Serukamba amesema mbio hizo zimepata heshima kubwa kwa mkoa wa Iringa kutokana na kuthibitishwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ndiye atakuwa mgeni rasmi katika tukio hilo la kitaifa.
“Hii ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Iringa na uthibitisho wa namna Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyounga mkono juhudi za michezo, utalii na maendeleo ya mikoa ya pembezoni,” amesema Serukamba.

Ameongeza kuwa Iringa sasa imefunguka kwa usafiri wa anga, ambapo mashirika ya ndege kama ATCL, Auric Air na Precision Air yanafanya safari za mara kwa mara kupitia viwanja vya ndege vya Nduli na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hivyo kuwawezesha wageni kufika kwa urahisi.
Aidha, aliwaalika wadau wa sekta binafsi na umma hasa katika maeneo ya huduma za malazi, chakula na usafiri kushiriki kikamilifu kwa kutoa huduma bora kwa wageni ili kuhakikisha mafanikio ya mbio hizo yanawanufaisha kiuchumi wananchi wa mkoa huo.
Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo, Hamim Kilahama, amesema kuwa Great Ruaha Marathon inalenga kutangaza utalii wa nyanda za juu kusini na kuhamasisha utunzaji wa mazingira, hususan uhifadhi wa Mto Ruaha ambao ni chanzo kikuu cha maji kwa taifa zima.
“Mwaka huu tumeongeza vionjo vya kipekee, vikiwemo ‘walking safari’ kwa wale wasiopendelea kukimbia pamoja na mashindano ya uvuvi (fishing competition),” amesema Kilahama, akibainisha kuwa gharama ya usajili ni shilingi 45,000 kwa kila mshiriki.
Naye Afisa Uhifadhi Daraja I wa Idara ya Utalii, Gaspar Athanas Kahabi, aliwahakikishia washiriki kuwa kutakuwa na ulinzi madhubuti ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambapo maafisa wa uhifadhi wamepangwa kila eneo ili kudhibiti wanyama na kuhakikisha usalama wa washiriki wote.
Mbio hizi si tu burudani ya michezo bali pia ni fursa ya kipekee ya kuutangaza mkoa wa Iringa kimataifa kupitia vivutio vyake vya kipekee vya utalii, historia na utamaduni.



