“Uchaguzi Mkuu uwape kipaumbele wanaothamini michezo”

IRINGA: Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, amewataka Watanzania kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 2025 unazaa viongozi watakaotoa kipaumbele kwa sekta ya michezo, sanaa na elimu ili kuibua vipaji vya vijana kitaifa na kimataifa.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yaliyofanyika katika shule ya sekondari Lugalo mjini Iringa, Kipanga amesema sekta ya michezo inahitaji viongozi wanaoielewa na kuitanguliza mbele kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kijana wa Kitanzania.

Kauli mbiu ya mwaka huu “Viongozi bora ni msingi wa maendeleo ya taaluma, sanaa na michezo — shiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu” imeakisi dhamira ya mashindano hayo yaliyohusisha wanamichezo 3,215 kutoka mikoa mbalimbali — wavulana 1,618 na wasichana 1,597 — pamoja na walimu, waratibu, waamuzi na kamati ya kitaifa.

Michezo iliyoshindaniwa ni pamoja na soka, netiboli, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, kriketi, mikono na sanaa za maonyesho kama vile kwaya, ngoma na muziki wa kizazi kipya, huku nidhamu na usafi vikipewa kipaumbele maalum.

Kipanga alisisitiza kuwa toleo la 2023 la Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, linatambua rasmi mchango wa michezo na sanaa katika maendeleo ya watoto na vijana, na ni sehemu ya mitaala kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vya ualimu.

“Sanaa na michezo sio shughuli za burudani pekee, ni fursa rasmi ya kukuza akili, maadili, afya na kuandaa vijana kwa ushindani wa soko la ajira,” alisema Kipanga.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu na kuhamasisha ushirikiano wa wadau wote kufanikisha ndoto hii.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Tamisemi, Atupele Mwambene, alisema mashindano hayo yaliyodumu kwa siku 12, yamekuwa jukwaa la kuimarisha mshikamano wa kitaifa kwa wanafunzi, huku yakifungua ukurasa mpya wa mashindano ya sekondari yatakayoanza leo Juni 19 hadi 30 mwaka huu.

Kwa ujumla, tukio hilo limeonyesha uhusiano wa karibu kati ya michezo na siasa, ambapo viongozi wa kisasa wanatakiwa kuwa mabalozi wa vipaji, maendeleo ya vijana na mshikamano wa kitaifa kupitia michezo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button