Dar Star bingwa Samia, soka bonanza

DAR ES SALAAM: TIMU ya soka ya Dar Star ya Ilala imeibuka mabingwa Bonanza maalum la kuwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuiadhibu Upanga Magharibi kwa mabao 4-1 katika fainali iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Bonanza hilo lilishindanisha timu nane za vijana zilizofanyika kwa siku mbili, lilihidhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka kujionea vipaji vilivyopo wilayani humo.
Baada ya ushindi huo, Dar Star walikabidhiwa kombe, medali na Sh milioni 1 huku Upanga Magharibi walikabidhiwa medali na Sh 500000.
Nahodha wa Dar Star Nasir Skoba aliwashukuru waandaaji kwa kuwapa nafasi vijana kwa kusema bonanza hilo limewasaidia kupanua wigo wa mahusiano yao kwenye michezo.
Nahodha wa Upanga Magharibi, Patrick Paul alisema pamoja na kuadhibiwa katika mchezo huo lakini wameguswa na hamasa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambako wanamuahidi Rais Samia na kumuahidi kumpigia kura kwa wingi.
“Sisi vijana wa Upanga Magharibi tunamuahidi Rais Samia, Oktoba tunatiki, mama mitano tena,” alisema.
Mratibu wa bonanza hilo ambaye ni Katibu wa hamasa wa CCM Upanga Magharibi Khalil Karim madhumuni ya bonanza hilo ni kuwaasa vijana kumsapoti Rais Samia na kumuahidi kwamba Oktoba tunatiki.
Karim alisema bonanza hilo litakuwa muendelezo litakalofanyika kila mwaka kwa ukubwa zaidi kupitia taasisi yake ya Kik Football Foundation.
Karim alizitaja timu zilizoshiriki bonanza hilo ni Tambaza, MOI, Bodaboda, Kalenga, Mchikichini Ilala, Kariakoo, Upanga Magharibi na Dar Star.
Karim alisema kauli mbiu ya bonanza hilo “Vijana Upanga Magharibi Samia/Zungu Oktoba tunatiki”. Aliweka bayana wadhamini wa bonanza hilo ni Car Spa, G1 Security, Evolve Health, Speed Sports, Afya, Fruttie na Rahim Cars.



