Taasisi yafanikisba bonanza ‘Asante Mama Super Cu’

DAR ES SALAAM: TAASISI ya KIK Football Foundation kwa kushirikiana na mdhamini mkuu State Group Holdings Ltd wamefanikisha Bonanza la Asante Mama Super Cup lililoanza Juni 21-22, 2025 katika viwanja vya Speed Sports – Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Bonanza hilo lililenga kumpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika maendeleo ya taifa, hususan kwa vijana na michezo.
Mkurugenzi wa KIK Football Foundation, Khalil Karim, alipongeza ushiriki mkubwa wa vijana na wadau wa michezo, huku akiahidi kuendeleza mashindano haya kila mwaka kwa kiwango kikubwa zaidi.
Katika bonanza hilo timu ya soka ya Dar Star ya Ilala iliibuka mabingwa Bonanza maalum la kuwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuiadhibu Upanga Magharibi kwa mabao 4-1 katika fainali iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Bonanza hilo lilishindanisha
timu nane za vijana zilizofanyika kwa siku mbili, lilihidhuriwa na idadi kubwa ya mashabiki wa soka kujionea vipaji vilivyopo wilayani humo.
Baada ya ushindi huo Dar Star walikabidhiwa kombe, medali na Sh milioni moja huku Upanga Magharibi walikabidhiwa medali na Sh 500000.
Nahodha wa Dar Star Nasir Skoba aliwashukuru waandaaji kwa kuwapa nafasi vijana.
Skoba alisema bonanza hilo limewasaidia kupanua wigo wa mahusiano ya michezo.
Kocha wa Dar Star Hussein Bakari alisema aliwaandaa vijana kubeba taji hilo.
“Sisi vijana wa Upanga Magharibi tunamuahidi Rais Samia, Oktoba tunatiki, mama mitano tena,” alisema.
Kocha wa Upanga Magharibi Juma Abbas bonanza hilo lilikuwa na ushindani wa aina yake.
Mratibu wa bonanza hilo ambaye ni Katibu wa hamasa wa CCM Upanga Magharibi Khalil Karim alisema madhumuni ya bonanza hilo ni kuwaasa vijana kumsapoti Rais Samia.
Karim alisema bonanza hilo litakuwa muendelezo litakalofanyika kila mwaka kwa ukubwa zaidi kupitia taasisi yake ya Kik Football Foundation.
Karim alizitaja timu zilizoshiriki bonanza hilo ni Tambaza, MOI, Bodaboda, Kalenga, Mchikichini Ilala, Kariakoo, Upanga Magharibi na Dar Star.



