Watoto Milioni 15.7 Wabaki Bila Chanjo

UINGEREZA : JUHUDI za utoaji chanjo kwa watoto duniani zimeripotiwa kusuasua tangu mwaka 2010, hali inayoweka mamilioni ya watoto katika hatari ya kuambukizwa magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.
Kwa mujibu wa ripoti mpya iliyochapishwa na Jarida la Afya la The Lancet limesema kiwango cha chanjo dhidi ya magonjwa kama surua, polio, kifua kikuu na tetenasi kimeshuka katika mataifa mengi, hali inayochangia kuendelea kwa maambukizi ya magonjwa hayo.
Takwimu za utafiti huo zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2023, zaidi ya watoto milioni 15.7 duniani hawakupata chanjo hata moja. Nusu ya watoto hao wanatoka katika nchi nane ambazo ni Nigeria, India, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Somalia, Sudan, Indonesia na Brazil.
Watafiti kutoka Taasisi ya Vipimo na Tathmini ya Afya ya Chuo Kikuu cha Washington wamebainisha kuwa ukosefu wa taarifa sahihi kwa wazazi umechangia kwa kiasi kikubwa wazazi wengi kushindwa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo muhimu.
Wataalamu wa afya wamesema hali hiyo inahatarisha mafanikio ya kimataifa katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, na kutoa wito wa kuwepo kwa mikakati mipya ya uhamasishaji, utoaji wa elimu kwa jamii na kuboresha huduma za afya hususan kwa watoto wadogo.



