MKOA wa Geita umefanikiwa kutoa chanjo zote muhimu kwa watoto 67,084 sawa na asilimia 51.6 ya lengo la kutoa chanjo zote kwa watoto 129,835 wenye umri chini ya miaka mitano kwa mwaka 2023.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe alieleza hayo juzi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kimkoa yaliyofanyika mjini Geita.
Alisema takwimu hizo ni kwa kipindi cha miezi mitano pekee kuanzia Januari mpaka Mei mwaka huu na juhudi zinaendelea kuhakikisha lengo linafikiwa ili kuimarisha usalama wa afya ya watoto.
Alibainisha mbali na watoto hao waliopatiwa chanjo zote muhimu, watoto 79,032 wenye umri wa miaka 2.5 wamepatiwa chanjo ya kuwakinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa surua.
Alieleza pia juhudi zinafanyika kumlinda mtoto wa kike dhidi ya maradhi hatarishi ambapo ndani ya miezi mitano mwaka huu mabinti 24,966 wamepatiwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.
Alisema hayo ni matokeo ya maboresho ya vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa hadi sasa mkoa una hospitali tisa, vituo vya afya 33 na zahanati 168 kati ya mahitaji ya hospitali 11, zahanati 237 na vituo vya afya 44.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Magembe Jackson alisema serikali kwa kushirikiana na wadau imejipanga kujenga miundombinu rafiki ya kutolea huduma za elimu na afya maeneo yote.