KCMC yasaka bilioni 2 kukamilisha ujenzi kituo cha moyo

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Rufaa Kanda ya Kaskazini (KCMC) imeanzisha mchakato wa kukusanya shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo kikubwa cha magonjwa ya moyo kitakachokuwa cha pili Tanzania baada ya JKCI.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga, amesema taasisi hiyo ya moyo itawasaidia wananchi wengi na kuipunguzia mzigo taasisi ya JKCI ya jijini dar es salaam.

Amesema mpaka sasa ujenzi wa kituo hicho umefikia aslimia 35 na tayari wapo wataalam waliotoka masomoni nje ya nchi wanasubiri kukamilika kwa ujenzi wake waanze kufanya kazi.

“Mpaka kituo hiki kikamilike ujenzi wake zinahitajika shilingi bilioni 22.5, lakini mpaka sasa wadau wetu kutoka nje ya Tanzania wametusaidia asilimia 90 ya gharama hizo.., palipobakia ni asilimia 10 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.7,” amesema Profesa Masenga.

Aidha, amesema kuwa fedha hizo wanategemea kuzipata kupitia michango ya watanzania na ndio sababu wamekuja na mkakati wa kuomba michango kumalizia kiasi hicho kilichobakia.

“Huko nyuma kulikuwa na mpango huu kupitia kwa mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi ambaye alitaka kujengwa kwa kituo hiki, lakini bahati mbaya mipango yake iliishia njiani kutokana na kifo chake. Mpango wetu wa sasa ni kuhakikisha mpaka kufika Julai mwaka 2027 jengo hilo liwe limakamilika na kuanza kutumika.” amesema Masenga.

“Kuna wataalamu ambao walienda kusoma nje masuala ya moyo, wapo walioenda kupitia mpango wa ‘Samia Scholarship’ na tayari wamerejea, mara baada ya jengo hili kuanza kazi hatutakuwa na shida ya wataala kwa sababu tayari wapo,” ameongeza Profesa Masenga.

Amesema tayari wametoa namba za simu na akaunti maalum kwa ajili ya kuchangia ambapo fedha zitaenda kwenye mradi huo moja kwa moja na kuwaomba watanzania kuchangia.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, Ronald Mbwasi, amesema kituo hicho kikikamilika kitatibu magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

“Asilimia 70 ya vifo duniani vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza na kati ya hayo asilimia 80 ni magonjwa ya moyo.., hapa ndipo tunapoona umuhimu wa ujenzi w akituo hiki ambacho si tu kitawasaidia wananchi wa kaskazini, bali kwa watanzania wote,” amesema Mbwasi.

Amesema watu wengi wa magonjwa ya moyo wanapoteza maisha kwa sababu umbali wa kufuata huduma lakini gharama za matibabu yake hivyo ujenzi huo utasaidia sana kwa wananchi.

“Kwa mfano kumsafirisha mgonjwa wa moyo anayehitaji matibabu ya haraka kwa ndege si chini ya dola 7000, wananchi wengi hawawezi kumudu, kukamilika kwa ujenzi huu kutasaidia sana kunusuru maisha ya watanzania kwa ukanda wa kaskazini na maeneo mingine,” amesema Mbwasi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanlink Health Care ambao wanashirikiana na KCMC kutafuta fedha za kukamilisha mradi huo, Dk. Siraj Mtulia, aliwataka watanzania kulibeba jambo hilo kitaifa na kufanikisha kukamilika ujenzi huo.

“Kituo hiki kikikamilika kinaenda kuwasaidia watanzania wote, tuawasaidie KCMC kukamilisha ujenzi,” amesema Mtulia.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button