Kikoti ajitosa tena ubunge Kilolo

IRINGA: Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kutoka Wilaya ya Kilolo, Brian Kikoti, leo amechukua rasmi fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Kilolo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiahidi kuwa daraja la mageuzi ya maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.

Kikoti, ambaye mwaka 2020 aliibuka nafasi ya pili katika mchakato wa kura za maoni za CCM katika jimbo hilo, amerejea tena safari hii akisisitiza kuwa ana ndoto kubwa ya kuliondoa Jimbo la Kilolo kwenye hatua za kawaida za maendeleo na kulifikisha hatua za juu zaidi kwa ushirikiano wa karibu na wananchi.

“Kilolo ni hazina ya fursa za maendeleo—kutoka kilimo, elimu, afya hadi utalii wa asili—zinahitaji usimamizi thabiti na mshikamano wa kweli na wananchi. Nina dhamira ya kuzikomboa fursa hizi na kuzifanya ziwe na tija kwa kila mkaazi wa Kilolo,” alisema Kikoti mara baada ya kuchukua fomu hiyo.

Amesisitiza kuwa anajivunia utumishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DK Samia Suluhu Hassan, akisema ameweka msingi imara wa maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ndani ya Kilolo na nchi nzima.

“Rais wetu Mama Samia ametuonyesha mwelekeo sahihi wa maendeleo kupitia Ilani ya CCM, nami nipo tayari kuendeleza kasi hiyo kwa vitendo kupitia bunge,” aliongeza kwa kujiamini.

Uchukuaji wa fomu hiyo ni sehemu ya mchakato wa awali wa ndani ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wanajitokeza kuchukua fomu kama ishara ya utayari wao kuitumikia jamii kupitia chama hicho.

Kwa historia yake ya uaminifu ndani ya chama, uzoefu wa kisiasa, na ndoto ya kuona Kilolo mpya, Kikoti anaonekana kuwa mmoja wa wagombea wanaopaswa kuangaliwa kwa jicho la matumaini na ushindani wa kweli.

Pamoja na Kikoti kuna wagombea wengine 20 akiwemo Mbunge anayemaliza muda wake, Justine Nyamoga wamechukua fomu za kuwania jimbo hilo kupitia chama hicho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button