Ngajilo apokelewa Iringa, atangaza kikao na wenyeviti wa mitaa

IRINGA: Mbunge mpya wa Iringa Mjini, Fabian Ngajilo, amepokelewa na wananchi wa jimbo hilo, tayari kwa kuanza rasmi majukumu yake akisisitiza ajenda ya amani, umoja na maridhiano.

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza katika ofisi za CCM Mkoa wa Iringa kumpokea, Ngajilo aliweka wazi shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kuanzisha Tume ya Maridhiano, akisema chombo hicho ni nguzo muhimu ya kujenga mazingira ya kisiasa yenye utulivu na kuimarisha mshikamano wa Taifa.
“Uamuzi wa Rais kuanzisha Tume ya Maridhiano ni hatua ya uongozi wenye busara. Bila amani hakuna maendeleo, na Rais Samia amethibitisha kuwa kinara wa utulivu,” alisema Ngajilo.
Aidha, aliwashukuru wananchi wa Iringa Mjini kwa kumwamini na kumpa kura nyingi, sambamba na kumpongeza Rais Samia kwa kuibuka na ushindi mkubwa katika Jimbo hilo.

“Sijajiweka mimi—nimewekwa na ninyi. Heshima mliyonipa ni kazi, na kazi hiyo nitailipa kwa bidii, ushirikiano na uwazi,” alisema.
Katika kujenga uongozi wa karibu na wananchi wa jimbo lake, Ngajilo amefichua mpango wake wa kuanzisha dawati la Wanawake, litakaloongozwa na mwanamke mwenye uzoefu wa kuchakata kero.
Lakini pia amesema ofisi yake itakuwa shirikishi yenye makatibu watatu akiwemo katibu wa mbunge – atakayeratibu shughuli za mbunge na kupokea kero za wananchi.
Wengine ni katibu wa siasa – atakaye kuwa na jukumu la kuunganisha ofisi ya mbunge na shughuli zote za kisiasa na katibu wa masuala ya kijamii – atakayekuwa akishughulikia changamoto na matukio ya kijamii
Aidha ameahidi ushirikiano wa karibu na meya, naibu meya, watendaji wote wa halmashauri, wenyeviti wa mitaa na mabalozi wa CCM.
Amesema kikao chake cha kwanza kitakuwa na wenyeviti wa mitaa ili kupata taswira ya changamoto za wananchi moja kwa moja kutoka ngazi ya chini.



