Salome arudisha fomu ubunge Viti Maalum

SHINYANGA: ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Salome Makamba, amerudisha fomu ya kugombea nafasi ya ubunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Shinyanga.
Makamba amerejesha fomu hiyo ikiwa ni sehemu ya mchakato wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Makamba alisema kwa sasa si wakati wa kutoa ahadi au kueleza matarajio, bali ni muda wa kufuata taratibu na maelekezo ya chama chake.

“Wakati ukifika nitasema. Ila kwa sasa ni wakati wa kufuata maelekezo ya Chama chetu pendwa cha Mapinduzi CCM na kuacha vikao vya maoni, mapendekezo na uteuzi vifanye kazi yake,” alisema Makamba.
Salome Makamba aliwahi kuhudumu kama Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA kabla ya kuhamia CCM, ambako sasa ameanza safari ya kutetea nafasi ya uongozi kwa kuwania ubunge kupitia kundi la wanawake wa UWT Mkoa wa Shinyanga.

